Habari

NAIBU WAZIRI PINDA AHIMIZA KULIPA KODI YA ARDHI

  • 03 Jun, 2024
NAIBU WAZIRI PINDA AHIMIZA KULIPA KODI YA ARDHI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewahimiza wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

Mhe Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Juni 204 alipokutana na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tangu Waziri wa Ardhi Mhe. Jerry Silaa kuwapa wamiliki wanaodaiwa kodi hiyo kuhakikisha wamelipa kodi kufikia juni 10, 2024.

 

"Naomba kusisitiza kwa wamiliki wote wa ardhi nchini, kutekeleza sharti la kulipa kodi ya ardhi kwa kuwa sasa tumeboresha njia za ukadiriaji na ulipaji wa kodi husika kidigitali". Amesema Mhe. Pinda.

 

Amewakumbusha wamiliki wa ardhi maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Waziri wa Ardhi Jerry Silaa  wakati wa kuhitmisha Hotuba ya Bajeti 2024 Bungeni kwamba, Wizara imedhamiria kuchukua hatua kwa wamiliki wote wa ardhi watakaoshindwa kutimizi masharti ikiwemo kuwafikisha mahakamani ili kuuza mali zao kufidia kodi ya ardhi na kupendekeza ubatilisho wa milki zao.

 

Amesema, wamiliki wa ardhi wanaweza kupokea Ankara za malipo kupitia ofisi za ardhi za mikoa na halmashauri na mara baada ya kupata makadirio ya kodi wanayodaiwa wanaweza kulipa kupitia benki au mawakala wa benki sambamba na njia ya simu ya kiganjani kwa kufuata taratibu za miamala ya malipo ya Serikali kupitia simu. 

 

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi amefafanua kuwa, malipo ya Kodi ya Pango la Ardhi hufanyika kwa kuzingatia ukubwa wa ardhi inayomilikishwa, matumizi ya ardhi yaliyoidhinishwa, thamani ya ardhi na kiwango cha malipo ya mbele (premium) ya ardhi inayomilikishwa. 

 

Mhe, Pinda amewataka wamiliki wa ardhi waliopimiwa ardhi kuhakikisha wanakwenda ofisi za ardhi kwa ajili ya kumilikishwa kwa kuwa wasipofanya hivyo baada ya siku tisini wataingizwa kwenye mfumo na kuanza kudaiwa kama wamiliki wengine.

 

Mhe. Pinda amegusia pia mkanganyiko uliopo baina ya kodi ya pango la ardhi na kodi ya majengo ambapo amesema Kodi ya Pango la ardhi hutozwa kwa wamiliki wa ardhi tofauti na Kodi ya Majengo ambayo hutozwa kwenye majengo/nyumba na kuwekewa utaratibu wa ulipaji na ukusanyaji wake ambapo kwa sasa inalipwa kwa njia ya malipo ya ununuaji wa umeme kupitia mfumo wa LUKU.