Habari
NAIBU WAZIRI MMUYA KUSHIRIKI MKUTANO MKUU WA MWAKA WA 45 WA TAASISI YA SHELTER AFRIQUE MOROCCO
- 09 Jun, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Kaspar Mmuya anatarajia kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa 45 wa Benki ya Maendeleo ya Makazi Afrika (Shelter Afrique Development Bank-ShafDB) utakaofanyika kuanzia Juni 9 hadi 12, 2026 jijini Rabat nchini Morocco.
Mkutano huo wa siku nne utaongozwa na kauli mbiu isemayo "Mustakabali wa Miji: Kugharamia Maendeleo ya Miji Jumuishi, ya Kijani na Yanayohimili Mabadiliko ya Tabianchi," ikilenga kujadili mbinu bunifu za upatikanaji wa mitaji kutoka masoko ya kimataifa na sekta binafsi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za makazi na miundombinu ya mijini Barani Afrika.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya atashiriki Mjadala Maalumu wa Mawaziri ambapo atawasilisha mada kuhusu uzoefu na mikakati ya Tanzania katika kuimarisha sekta ya makazi, mipango miji na maendeleo endelevu ya miji.
Aidha, Mhe Mmuya na ujumbe wake watapata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati ya miji ya kijani nchini Morocco kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, uendelezaji makazi jumuishi na uboreshaji wa makazi yasiyo rasmi.
Kupitia ushiriki wa mkutano huo, Tanzania inatarajia kuimarisha ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Shelter Afrique na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kupanua fursa za upatikanaji mikopo, uwekezaji pamoja na misaada ya kiufundi.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo unajumuisha Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Upendo Matotola pamoja na wawakilishi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), na Kampuni ya Soko la Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC).
Shelter Afrique ni taasisi ya fedha inayoundwa na Serikali za Africa kwa kushirikiana na Benki ya Africa zinazochangia mtaji kwa kununua hisa na kujenga mtaji unaotumiwa na nchi wanachama katika shughuli za Maendeleo ya Nyumba na Miji Afrika.