Habari

NAIBU WAZIRI MMUYA ATUNUKU VYETI VYA USAJILI KWA WATHAMINI 38

  • 26 Oct, 2026
NAIBU WAZIRI MMUYA ATUNUKU VYETI VYA USAJILI KWA WATHAMINI 38

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ametunuku vyeti vya usajili kwa wathamini 38 katika Mahafali ya Tano ya Bodi ya Usajili wa Wathamini yaliyofanyika tarehe 22 Oktoba 2026, katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mmuya amewataka wathamini hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, uadilifu na misingi ya taaluma, akisisitiza umuhimu wa kutoa tathmini sahihi na zenye kuzingatia viwango na taratibu zilizowekwa. Amesema taaluma ya uthamini ina nafasi muhimu katika sekta ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, hususan katika kusaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu thamani ya mali na uwekezaji.

 

Aidha, amewahimiza wathamini hao kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika kuboresha huduma za uthamini nchini, kuzingatia maadili ya taaluma na kuepuka vitendo vinavyoweza kuathiri uaminifu wa taarifa za uthamini. Amewataka pia kuendelea kujifunza na kuendana na mabadiliko ya kitaaluma na kiteknolojia ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma wanazozitoa kwa wananchi, taasisi na wadau wa sekta mbalimbali.

 

Mahafali hayo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza taaluma ya uthamini nchini kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinafanywa na wataalamu waliosajiliwa na wenye kuzingatia viwango vya kitaaluma. Uwepo wa wathamini wenye weledi na uadilifu ni muhimu katika kuimarisha imani ya wananchi na wawekezaji katika taarifa za thamani ya mali, pamoja na kusaidia maendeleo endelevu ya sekta ya ardhi na nyumba.