Habari
NAIBU WAZIRI MMUYA AAGIZA CHARNJEET APEWE HATI YAKE MAKAMBAKO
- 12 May, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya ameielekeza Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Njombe kumkabidhi Bwn. Charnjeet Singh SahotaHati ya Hakimiliki ya kiwanja Na. 75 Kitalu P Makambako baada ya kubainika kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo hilo ambalo lilikuwa linaingiliwa na watu waliotaka kujimilikisha kinyume cha sheria.
Mhe. Mmuya ametoa kauli katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika katika viwanja vya polisi Makambako mkoani Njombe tarehe 09 Mei 2026. Maelekezo hayo yamekuja kufuatia mgogoro wa muda mrefu uliolenga kupora ardhi ya familia hiyo, kitendo kilichofanyika wakati Bwana Charnjeet akiwa anakabiliwa na changamoto za kisheria na kuwekwa kizuizini.
inaelezwa kuwa bwana Charnjeet Singh Sahota mmiliki wa eneo hilo mara baada ya kupata changamoto za kisheria na kuwekwa kizuizini ndipo majirani zake waliamua kujimilikisha eneo hilo pasipo kufuata taratibu rasmi kiasi cha kufikia kuanza kuliuza.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Mji Makambako Bi. Flaviana Mamkwe amesema kuwa Charnjeet alirithi eneo hilo kutoka kwa marehemu baba yake, ambaye awali alinunua kutoka kwa mtu aliyefahamika kwa jina la Habibu Mwaligoye Hata hivyo, mara baada ya Charnjeet kufungwa gerezani, muuzaji huyo (Habibu) aliibuka tena na kudai kuwa eneo ni lake licha ya kuwa alishauza na kupokea malipo miaka mingi iliyopita.
Ziara ya Naibu Waziri Mkoani Njombe ilikuwa na lengo la kusikiliza hoja mbalimbali za wananchi juu ya masuala ya ardhi, kuzungumza na wataalamu wa Ardhi ili kujenga uelewa wa pamoja wa kutekeleza majukumu yao, kukabidhi Hati za Hakimiliki za Ardhi sambamba na kuhamasisha ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi.