Habari

NAIBU WAZIRI MKUU BITEKO AWATAKA WATANZANIA KUTAMBUA KUWA RASILIMALI ARDHI NI UTAJIRI

  • 13 Sep, 2023
NAIBU WAZIRI MKUU BITEKO AWATAKA WATANZANIA KUTAMBUA KUWA RASILIMALI ARDHI NI UTAJIRI

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri wa Nishati Dkt. Doto  Mashaka Biteko amewataka watanzania kutambua kuwa ukiachana na teknlojia utajili uliobaki unatokana na rasimali ardhi hivyo kuwataka  kuwa na hatimiliki ya ardhi ili waweze kuneemeka na rasilimali hiyo.

Dkt. Biteko amesema hayo jana tarehe 12 septemba 23 alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Kimataifa la Taasisi za Ardhi Afrika linaloendelea kwa siku tatu jijini Arusha.

 Aidha Dkt. Biteko amewataka  watanzania kuhakisha wanatumia   wataalamu wa sekta ardhi nchini  ili wasaidie kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo hapa Nchini.

"Usikubali kuwa na kipande cha ardhi bila kuwa na hati yake watafute wataalamu wetu wakupima, wakupangie na hatimaye wakumilikishe ardhi hiyo ili uweze kujiletea Maendeleo". Aliongeza Dkt. Biteko Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Doto Biteko aliongeza kuwa watanzania wanatakiwa kuwa na ardhi na hivyo wanapaswa kuitunza na kujipatia hatimilki kwa ajili ya uhalali wa kumiliki ardhi hiyo.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amesema kuwa katiba ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya kila Mtanzania Kumiliki ardhi kwani sera na sheria za ardhi nchini zimewahakikishia wananchi kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Waziri Silaa aliongeza kuwa Katiba ya nchi inatoa haki sawa kwa watanzania kumiliki ardhi pia sera na sheria za ardhi nchini zimewahakikishia wananchi wote upatikanaji wa hakimiliki za ardhi kwa lengo la uzalishaji mali na kujipatia kwa maendeleo.

Waziri Silaa katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo aliongeza  kuwa ustawi wa ardhi nchini umekuwa ni msingi wa Maendeleo ya sekta nyingine za kiuchumi.

Aidha kiongozi huyo alibainisha kwa upangaji mzuri wa miji na majiji umewezesha ujenzi wa mtandao wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege nchi nzima na maendeleo hayo ya miundombinu yamewezesha ustawi wa sekta nyingine ikiwemo utalii nchini.

Aidha Waziri Silaa amebainisha changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi barani Afrika zinatokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, ongezeka la idadi ya watu, upungufu wa rasilimali fedha na wataalamu na mahitaji makubwa ya matumizi ya ardhi ilihali ardhi haiongezeki.

Kongamani hili lenye agenda kuu ya upatikanaji wa hakimiliki za ardhi kwa wananchi linafanyika kwa mara ya kwanza hapa Nchini na kuhudhuriwa na  na nchi takribani 21 na Taasisi za ardhi  13 kutoka bara la Afrika.