Habari
MWANZA YAJA NA KLINIKI YA ARDHI KATA KWA KATA KUWAFIKIA WATU KWENYE MAENEO YAO
- 13 Sep, 2024
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kutoa huduma kwenye sekta ya Ardhi kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapangwa, kinapimwa na kumilikishwa.
Akikabidhi Hati Miliki za ardhi kwa wananchi wa Kata ya Pansiansi Mkoani Mwanza
Septemba 13, 2024, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoani humo Bi. Happiness Mtutwa amesema ofisi yake imesogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kupitia Kliniki ya Ardhi ambayo hufanyika kata kwa kata mkoni humo kila siku ya Ijumaa.
"Lengo tunatamani kila mwananchi mwenye kero inayohusiana na ardhi tuitatue na wenye migogoro pia tunatafuta suluhu. Kwa wale wenye malalamiko tunayamaliza kabisa kwa sababu tulibaini wananchi wetu wengi changamoto yao kubwa ni kupata hati" Bi. Mtutwa
Ameongeza kuwa jukumu lao ni kuwasikiliza wananchi na kupatia majawabu na ufumbuzi wa changamoto za ardhi zinazowakabili katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanakamilisha zoezi zima la kumilikisha ardhi kwa kuwapatia Hati Miliki katika maeneo yao.
Naye Diwani wa Kata hiyo Bi. Rosemary Mayunga ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuendesha zoezi la kliniki ya Ardhi kata kwa kata hatua inayowapunguzia mzigo wananchi.
"Tunapongeza serikali yetu sikivu ina utayari wa kuhudumia wananchi wao, ina utayari wa kusogeza huduma kwa wananchi kwa sababu wananchi hawa walikuwa wanafata huduma wanatembea wanarudi lakini kwenye hili kwetu ni faraja" amesema Bi. Mayunga.
Kwa upande wake Francis Mageto mkazi wa kata ya Pansiansi amesema kwa sasa huduma za ardhi zimerahisishwa kwa kuwa huduma hiyo imesogezwa karibu na makazi yao huku akisifu mchakato wa upatikanaji wa hati.
"Najisikia furaha sana kupata hati maana ilikuwa sio rahisi, kwa hiyo mimi naona furaha kupata hati kirahisi hivi, serikali ya Mama Samia mimi naielewa sana" amesema Bw. Mageto.
Zoezi hilo katika kata ya Pansiansi Mkoani Mwanza linafanywa kwa ushirikiano wa Maafisa Ardhi wakati wa Kliniki ya Ardhi ya kata kwa kata kwa uratibu wa Ofisi ya Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza na Ofisi ya Mkurugenzi jiji la Mwanza ambayo hufanyika kila Ijumaa kwa kuzunguka kwenye kata za jiji hilo.