Habari

MWANANCHI NJOMBE AFURAHISHWA NA HUDUMA YA e-ARDHI, APATA HATI NDANI YA SIKU MOJA

  • 21 Sep, 2026
MWANANCHI NJOMBE AFURAHISHWA NA HUDUMA YA e-ARDHI, APATA HATI NDANI YA SIKU MOJA

Mwananchi kutoka Halmashauri ya Ludewa mkoani Njombe, Bw. Leonard Paul Ngimba, ameonesha kuridhishwa na matumizi ya mfumo wa e-Ardhi baada ya kufungua maombi ya hati ya umiliki wa ardhi kupitia mfumo huo na kukamilishiwa huduma ndani ya siku moja.

 

Leonard ameyasema hayo leo, Septemba 20, 2026, mkoani Njombe wakati akikabidhiwa hati yake ya umiliki wa ardhi iliyoandaliwa na kutolewa kwa kutumia mfumo wa e-Ardhi.

 

Amesema aliweza kufungua akaunti na kuwasilisha maombi mwenyewe kupitia mfumo huo na baadaye kufika ofisi za ardhi mkoa kwa ajili ya kuchukua hati yake baada ya kukamilishwa.

 

“Nimeomba mwenyewe kwenye mfumo wa e-Ardhi, nimefungua akaunti na maombi nimefanyia kulekule. Nimefika kuchukua hati tu,” amesema Leonard.

 

Amesema matumizi ya mfumo huo yamerahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa kupunguza muda anaotumia mwananchi kufuatilia huduma hiyo, huku akiwahimiza wananchi wengine kutumia mfumo huo.

 

Leonard ameongeza kuwa, mfumo wa e-Ardhi unawapa wananchi fursa ya kuanzisha na kufuatilia maombi ya huduma za ardhi kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika ofisini mara kwa mara, hivyo kuokoa muda na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

 

Kwa upande wa Mkoa wa Njombe, hadi sasa umekamilisha jumla ya hati 13 tayari kwa ajili ya kukabidhiwa wananchi, ambapo hati 2 tayari zimekabidhiwa. 

 

Wananchi ambao wako nje ya Mkoa wa Njombe wamejulishwa kuwa wanaweza kuchukua hati zao katika ofisi za ardhi za mikoa waliopo.

 

Mfumo wa e-Ardhi ni miongoni mwa jitihada za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za kutumia teknolojia ya kidijiti kuboresha utoaji wa huduma za ardhi, kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.