Habari

MTWARA KUCHELE! MAFUNZO YA MFUMO WA e-ARDHI YAANZA KWA KISHINDO

  • 21 Sep, 2026
MTWARA KUCHELE! MAFUNZO YA MFUMO WA e-ARDHI YAANZA KWA KISHINDO

Mafunzo ya Mfumo wa e-Ardhi yameanza mkoani Mtwara, huku wataalamu wa masuala ya ardhi wakijipanga kutumia mfumo huo wa kidijiti katika kuboresha utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi kwa weledi, ufanisi na kwa wakati.

 

Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wataalamu wa ardhi kupata uelewa na ujuzi wa kutumia Mfumo wa e-Ardhi, hatua inayotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi na kuongeza ufanisi katika kushughulikia mahitaji ya wananchi.

 

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mpima Ardhi kutoka Ofisi ya Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Bw. Abdalla Komba, amesema wamepokea mafunzo hayo kwa moyo wa dhati, akieleza kuwa mfumo huo utawasaidia wataalamu kurahisisha na kuboresha huduma za ardhi kwa wananchi mkoani Mtwara.

 

 “Tumepokea mafunzo haya kwa moyo wa dhati kwa sababu yatatusaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa wananchi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi zaidi,” amesema Komba.

 

Aidha, amewahimiza wananchi mkoani Mtwara kutumia fursa ya Mfumo wa e-Ardhi kwa kuanza kuomba hati za ardhi kiganjani, huku akiwataka wale watakaohitaji msaada katika kutumia mfumo huo kufika katika ofisi za ardhi za halmashauri au Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kupata huduma na maelekezo kutoka kwa wataalamu.

 

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijiti katika utoaji wa huduma za ardhi, kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupunguza urasimu na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi.