Habari

MRADI WA 'PAMOJA TUHIFADHI BAHARI YETU' WAWEZESHA WANANCHI KIJIJI CHA KIWAWA KUPATA HATI 426 ZA KIMILA

  • 01 Sep, 2026
MRADI WA 'PAMOJA TUHIFADHI BAHARI YETU' WAWEZESHA WANANCHI KIJIJI CHA KIWAWA KUPATA HATI 426 ZA KIMILA

Wananchi 426 wa Kijiji cha Kiwawa, Kata ya Mandawa, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, wamewezeshwa kupata Hati za Kimila kupitia Mradi wa “Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu”, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Uhifadhi Mazingira Duniani (WWF) na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi Mazingira (IUCN) na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

 

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa hati hizo iliyofanyika tarehe 31 Agosti 2026, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amewataka wananchi hao wa Kijiji Cha Kiwawa kuendelea kulinda na kutunza ardhi, misitu na mazingira ya bahari, akisisitiza kuwa uhifadhi wa rasilimali hizo ni msingi wa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

 

Mhe. Nyundo amesema upatikanaji wa hati hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa milki za wananchi, hivyo kuwataka kutumia fursa hiyo kulinda ardhi yao na kuhakikisha matumizi yake yanafanyika kwa kuzingatia sheria, taratibu na mipango ya matumizi bora ya ardhi.

 

Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Lindi, Bw. Geofrey Martin, amewapongeza wananchi wa Kiwawa kwa kushiriki kikamilifu zoezi hilo, huku akiwataka wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kusogeza huduma za upimaji na utoaji wa hati za kimila katika vijiji vingine.

 

Amezitaja baadhi ya changamoto zinazoweza kuchelewesha upatikanaji hati ni kuwa pamoja na wananchi kutokuwa na namba za utambulisho wa kiraia pamoja na migogoro ya mipaka.

 

Amewataka wananchi wa Kiwawa kufuata taratibu wanazoelekezwa na wataalamu wa ardhi ili kuhakikisha taarifa zao zinatambulika kisheria na kuimarisha usalama wa milki zao.

 

Naye Meneja Mradi, Bi. Hania Mkogas, amesema shirika WWF na IUCN wameendelea kushirikiana na Wizara ya Ardhi pamoja na wizara nyingine kuimarisha usimamizi endelevu wa ardhi, misitu na mazingira kupitia Mradi wa “Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu.”

 

Ameeleza kuwa, ushirikiano huo umewezesha wananchi wa Kiwawa kupata hati 426 zinazothibitisha umiliki wao na kusaidia kulinda haki zao za kumiliki ardhi.

 

Kwa upande wao Wananchi wa Kiwawa wameishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Umoja wa Ulaya, WWF na IUCN kwa kuwawezesha kukamilisha zoezi la upatikanaji hati hizo, wakieleza kuwa hati milki walizopata zitawasaidia kuimarisha usalama wa milki zao na kuweka msingi wa maendeleo kwao na vizazi vijavyo.