Habari

MMUYA: WAKURUGENZI LINDENI MAENEO YA WAZI

  • 01 Oct, 2026
MMUYA: WAKURUGENZI LINDENI MAENEO YA WAZI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha maeneo ya wazi yanalindwa kwa kuwekewa alama za kudumu na mabango yanayoonyesha mipaka akisisitiza kuwa maeneo hayo hayapaswi kubadilishiwa matumizi.

 

Mhe. Mmuya ametoa agizo hilo Septemba 30, 2026, wakati wa ziara ya kukagua mipango ya miji na upimaji wa ardhi katika Jiji la Dodoma, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za mapema kulinda maeneo ya wazi ili kuzuia migogoro ya ardhi na uvamizi.

 

Amesema Jiji la Dodoma lina jumla ya maeneo ya wazi 3,237 yaliyotengwa kwa matumizi mbalimbali ya umma, ikiwemo maeneo ya michezo, mapumziko, mazingira na maziko, lakini ni maeneo 385 pekee yenye hati.

 

“Maagizo yangu ni kwamba Wakurugenzi wote wanaomiliki maeneo ya wazi waweke alama za kudumu zinazoonekana pamoja na mabango makubwa yanayoonyesha eneo hilo lina ukubwa gani, liko pale kwa matumizi gani na nani mmiliki,” amesema Mmuya.

 

Amesema katika ukaguzi uliofanyika maeneo matano ya wazi jijini Dodoma, ni eneo moja pekee lililobainika kuwa na hati, huku maeneo mengine yakiwa hayana mipaka inayoonekana wazi, hali ambayo amesema inaweza kusababisha migogoro kati ya Halmashauri na wavamizi wa maeneo hayo.

 

Mhe. Mmuya pia amesisitiza kuwa mabadiliko ya matumizi ya maeneo ya wazi hayapaswi kufanyika kinyume na taratibu zilizowekwa, akirejea Kanuni na Tangazo la Serikali (GN) Na. 91 la mwaka 2018, Kipengele cha Tatu, linaloweka masharti kuhusu matumizi ya maeneo ya wazi.