Habari

MMUYA: TUTAWATHIBITISHIA WATU KWA VITENDO, SI KWA MANENO, TUKAZE BUTI

  • 07 Sep, 2026
MMUYA: TUTAWATHIBITISHIA WATU KWA VITENDO, SI KWA MANENO, TUKAZE BUTI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka watumishi wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kutokata tamaa wala kuyumba kutokana na changamoto na maoni yanayotolewa kuhusu utendaji wa chuo hicho, bali kutumia maoni hayo kama fursa ya kujenga na kuboresha zaidi.

 

Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo leo Septemba 5, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa ARIMO mkoani Morogoro, akisisitiza umuhimu wa kusikiliza maoni, kufanya uchambuzi na kuyatumia katika kusonga mbele, huku akiwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na kuwa wazi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

“Yale yanayosemwa yasikieni, msiyapuuzuze, wekeni chini mfanye analysis, songeni mbele kwa kuboresha. Lakini msikate tamaa kwa kufanya mazuri tunayoyafanya. Watakuja kutusema kwa uzuri kama sisi tukiendelea kufanya mazuri,” amesema Mhe. Mmuya.

 

Amesema mafanikio ya ARIMO na sekta ya ardhi kwa ujumla yataonekana zaidi kupitia matokeo ya kazi, akiwataka watumishi kuendelea kuwathibitishia wananchi kwa vitendo badala ya kutumia muda mwingi kujibu changamoto na lawama zinazotolewa.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Veronica Hamis Mwambwaro, ameiomba Wizara ya Ardhi kusimamia kwa karibu mchakato wa uundaji wa mitaala, akieleza umuhimu wa kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya sasa na yajayo katika sekta ya ardhi.

 

Naye Najim Mchunda ameiomba Wizara kusaidia upatikanaji wa Land Laboratory (Land Lab), ambayo itatumika katika kufanya tafiti na kuhifadhi taarifa muhimu za ardhi zitakazosaidia katika utafiti na utoaji wa maarifa kwa sekta. 

 

Kwa upande wake, Mpoki Chengelera ameomba Wizara kusaidia upatikanaji wa {Server} kwa ajili ya kuhifadhi na kusimamia taarifa za ardhi zinazozalishwa na chuo, hususan data zinazokusanywa na wanafunzi wakati wa mafunzo ya vitendo na kazi za field.

 

Kikao hicho cha Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya na watumishi wa Chuo Cha Ardhi Morogoro ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Agosti 30, 2026 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ya kufika chuoni hapo kusikiliza changamoto zao.