Habari
MMUYA: SERIKALI YAJA NA MKAKATI WA KUDUMU KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI
- 26 Aug, 2026
SERIKALI imeanza hatua za kuandaa utaratibu wa kudumu wa kutatua migogoro ya ardhi nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha migogoro hiyo inapatiwa suluhisho kwa wakati na kwa ufanisi.
Akijibu swali Bungeni leo tarehe 26 Agost 2026 katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Nne, wa Bunge la 13, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi na tayari imeanza kuchukua hatua za kuimarisha utatuzi wake.
Amesema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alielekeza Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuandaa mapendekezo yatakayowezesha kupata suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi nchini.
Mhe. Mmuya amesema katika kutekeleza maelekezo hayo, Wizara kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali imeandaa Rasimu ya Mkakati wa Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Nchini, ambao utakapotekelezwa utasaidia kuimarisha uelewa, uwajibikaji na kasi katika kushughulikia migogoro ya ardhi.
Aidha. Amesema utekelezaji wa Mkakati huo unalenga pia kuimarisha amani, umoja na mshikamano katika jamii, pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika ardhi na kukuza uchumi wa nchi.