Habari
MMUYA: MFUMO WA E-ARDHI KUPUNGUZA MALALAMIKO NA MIANYA YA RUSHWA KATIKA HUDUMA ZA ARDHI
- 26 Oct, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Huduma za Ardhi (E-Ardhi) yanalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza uwazi na kupunguza mianya inayoweza kuchangia vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma za ardhi nchini.
Akizungumza tarehe 22 Oktoba 2026, katika Mahafali ya Tano ya Bodi ya Usajili wa Wathamini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhe. Mmuya ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za ardhi ni hatua muhimu katika kurahisisha taratibu za huduma, kuimarisha uwajibikaji na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma hizo.
Aidha, amewataka wananchi wanaotumia Mfumo wa E-Ardhi kuhakikisha wanatoa taarifa mapema pindi wanapokutana na changamoto yoyote katika matumizi ya mfumo huo, ili ziweze kufanyiwa kazi na mamlaka husika kwa wakati. Amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika kutoa mrejesho ni muhimu katika kuboresha mfumo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na mahitaji yao.
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na wataalamu wa sekta ya ardhi ni muhimu katika kuhakikisha changamoto za kiutendaji na kiteknolojia zinatambuliwa na kutatuliwa kwa wakati, huku wananchi wakihimizwa kutumia njia rasmi za mawasiliano na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyokwenda kinyume na taratibu za utoaji wa huduma.
Mhe. Mmuya amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya E-Ardhi, yakifuatana na uwajibikaji wa watumishi na mrejesho wa wananchi, yatasaidia kuimarisha uwazi, kuongeza ufanisi na kujenga imani ya wananchi katika huduma za ardhi nchini.