Habari
MMUYA: LINDA ARDHI YAKO, MUDA RAHISI WA KUPATA HATI NI SASA
- 02 Oct, 2026
★ Asema mifumo ya utoaji huduma imedhibiti watu kati ★ Akabidhi hati zaidi ya 800 za miliki za ardhi Mafinga
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema maboresho ya mifumo ya utoaji huduma za ardhi yamewezesha wananchi kupata hati za miliki kwa urahisi zaidi na kupunguza utegemezi wa watu kati katika upatikanaji wa huduma hizo.
Mhe. Mmuya ameyasema hayo Oktoba 1, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mashujaa, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, ambapo pia alikabidhi hati zaidi ya 800 za miliki za ardhi kwa wananchi.
Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za ardhi yamerahisisha wananchi kufuatilia huduma zao moja kwa moja, akiwataka wenye viwanja na ardhi zinazostahili kumilikishwa kutumia fursa hiyo kukamilisha taratibu za kupata hati.
Mhe. Mmuya amesisitiza kuwa hati ya miliki ni uthibitisho wa kisheria wa umiliki wa ardhi, hivyo wananchi wanaomiliki ardhi kihalali wanapaswa kuhakikisha wanakamilisha taratibu za umilikishaji ili kuimarisha usalama wa umiliki na kupunguza uwezekano wa migogoro.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Reuben Chongolo, amesema urasimishaji wa ardhi ni hatua muhimu katika kupunguza migogoro na kuwezesha wananchi kutumia ardhi yao kwa uhakika zaidi katika shughuli za uzalishaji.
Amesema uwepo wa mipango na umiliki rasmi wa ardhi unasaidia kuweka utaratibu katika matumizi ya ardhi na kupunguza migongano inayoweza kujitokeza miongoni mwa wananchi.
Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Bi. Rehema Kilonzo, amesema Kliniki za Ardhi zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi kwa ajili ya kutoa elimu, kusikiliza changamoto na kutoa huduma zinazohusiana na ardhi.
Halmashauri ya Mji wa Mafinga, inaonesha kuwa kuna jumla ya viwanja 21,776, ambapo 19,465 tayari vimeshamilikishwa na kuingizwa katika mfumo wa MOLIS. Aidha, zoezi la urasimishaji linaendelea katika mitaa 17, ambapo vipande 22,972 vimetambuliwa, viwanja 21,776 vimepangwa na viwanja 12,539 vimepimwa hadi sasa.