Habari

MMUYA: HESHIMUNI MIPAKA ILIYOPIMWA, TUONDOE MIGOGORO YA ARDHI

  • 25 Sep, 2026
MMUYA: HESHIMUNI MIPAKA ILIYOPIMWA, TUONDOE MIGOGORO YA ARDHI

Wananchi wametakiwa kuheshimu mipaka ya ardhi iliyopimwa na kutambuliwa kitaalamu, ambayo ni hatua muhimu katika kuzuia na kumaliza migogoro ya mipaka kati ya vijiji na maeneo mengine nchini.

 

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya ametoa kauli hiyo mara baada ya kusikiliza hoja na changamoto za wananchi wa Kata ya Nkowe, Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, ambapo alijibu hoja ya mwananchi kuhusu mgogoro wa mipaka kati ya Vijiji vya Nandenje na Kipindimbi.

 

Amesema wananchi wanapaswa kuachana na dhana ya kutegemea mipaka ya asili pale ambapo tayari mipaka imepimwa na kutambuliwa kitaalamu, kwa kuwa kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa vipimo na ramani kunaweka uelewa wa pamoja na kupunguza uwezekano wa migogoro kujitokeza.

 

“Kila kizazi kikija kizingatie mipaka hiyo katika maeneombalimbali, mambo ya asili yaliisha, tuzingatie mipaka iliyowekwa kitaalamu” amesema Mmuya.

 

Mhe. Mmuya amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha ardhi nchini inapangwa, inapimwa na kumilikishwa, akieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka shilingi bilioni 38 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kuharakisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji. 

 

Serikali inasisitiza kuwa kiasi hicho cha fedha tawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika zaidi ya vijiji 1,400. 

 

Naibu Waziri amesema hatua hiyo inalenga kuweka utaratibu unaoeleweka wa matumizi ya ardhi, kutambua maeneo ya vijiji na matumizi mbalimbali, pamoja na kupunguza migogoro inayotokana na kutokuwepo kwa mipaka na mipango ya matumizi ya ardhi. Wizara pia imeeleza kuwa upimaji na uwekaji wa mipaka ya wazi ni miongoni mwa hatua zinazolenga kupata suluhu ya kudumu ya migogoro ya ardhi nchini.

 

Mhe. Mmuya amewataka wananchi wa Nandenje na Kipindimbi kutumia taarifa za kitaalamu, ramani na alama rasmi za mipaka katika kushughulikia mgogoro huo, huku akiwasisitiza viongozi wa maeneo hayo kushirikiana na wataalamu wa ardhi ili kuhakikisha mipaka inayotambuliwa kisheria inaheshimiwa na kulindwa.