Habari

MMUYA AWATAKA WATHAMINI KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU THAMANI YA ARDHI NA MALI ZAO

  • 26 Oct, 2026
MMUYA AWATAKA WATHAMINI KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU THAMANI YA ARDHI NA MALI ZAO

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka wathamini nchini kutoa elimu kwa wananchi kuhusu thamani halisi ya ardhi na mali zao ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa mauziano ya ardhi.

 

Akizungumza tarehe 22 Oktoba 2026, katika Mahafali ya Tano ya Bodi ya Usajili wa Wathamini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhe. Mmuya amesema elimu hiyo ni muhimu kwa wananchi kuelewa thamani ya ardhi wanayomiliki kabla ya kufanya maamuzi ya kuiuza au kuitumia kwa shughuli nyingine za maendeleo.

 

Amesema baadhi ya vijiji vimekuwa vikiuza maeneo makubwa ya ardhi kwa watu wachache, hali inayoweza kupunguza maeneo yanayopatikana kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na mahitaji ya wananchi wa vijiji hivyo. Ameeleza kuwa changamoto hiyo inahitaji uelewa mpana wa thamani ya ardhi na mipango bora ya matumizi yake, ikizingatiwa kuwa idadi ya watu inaendelea kuongezeka huku ardhi ikiwa ni rasilimali isiyoongezeka.

 

Aidha, Mhe. Mmuya amewahimiza wathamini kuwaelimisha wananchi kuhusu uwezekano wa kutumia mifumo ya umiliki wa pamoja wa ardhi pale inapofaa na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo, badala ya kuuza ardhi yao moja kwa moja na kupoteza umiliki wake. Kupitia utaratibu huo, wamiliki wanaweza kuingia makubaliano yanayowatambua katika umiliki wa mali au mradi kwa uwiano uliokubaliwa, ikiwemo asilimia ya umiliki, kulingana na thamani ya ardhi wanayochangia.

 

Amesisitiza kuwa uelewa sahihi wa thamani ya ardhi na uwekaji wa makubaliano ya wazi unaweza kusaidia kupunguza migogoro inayotokana na mauziano ya ardhi. Amesema katika baadhi ya mazingira, wamiliki wamekuwa wakibadili msimamo baada ya kugundua kuwa ardhi waliyoahidi kuuza ina thamani kubwa kuliko walivyodhani, hali inayoweza kuvuruga makubaliano na kusababisha migogoro kati ya wahusika.

 

Amewataka wathamini kutumia utaalamu wao kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu thamani ya ardhi na mali zao, kuelewa chaguo mbalimbali za kiuchumi walizonazo na kufanya maamuzi yanayolinda maslahi yao ya sasa na ya baadaye. Hatua hiyo itasaidia kuimarisha matumizi endelevu ya ardhi, kulinda rasilimali za jamii na kuchangia maendeleo ya sekta ya ardhi na nyumba nchini.