Habari

MMUYA AWATAKA HALMASHAURI KUHAKIKISHA MAENEO YA SERIKALI YANAMILIKIWA KISHERIA

  • 21 Sep, 2026
MMUYA AWATAKA HALMASHAURI KUHAKIKISHA MAENEO YA SERIKALI YANAMILIKIWA KISHERIA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya nchini kuhakikisha maeneo ya Serikali na taasisi zake, ikiwemo maeneo ya wazi, yanapimwa na kumilikishwa kwa hati ili kulinda ardhi hiyo dhidi ya uvamizi na migogoro.

 

“Wakurugenzi wote, Wenyeviti wa Halmashauri zote, Mameya wote mna dhamana ya kumiliki maeneo yenu ya Serikali na taasisi zake zilizopo hapo, ikiwemo maeneo ya wazi,” amesema Mhe. Kaspar Mmuya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 

Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo leo, Septemba 18, 2026, muda mfupi baada ya kufungua mafunzo ya madini kwa wachimbaji, yaliyofanyika wakati wa Maonesho ya Madini Lindi 2026 yanayoendelea Wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi.

 

Hatua hiyo imefuatia ziara ya Mhe. Mmuya ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Chinongwe, Septemba 17, 2026, ambapo alibaini kuwa eneo hilo halikuwa na hati miliki licha ya kuwa taratibu muhimu za upimaji zilikuwa zimekamilika.

 

Baada ya kubaini hali hiyo, Mhe. Mmuya aliiagiza Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Ruangwa kukamilisha haraka taratibu zilizobaki za uandaaji wa hati, hatua ambayo imewezesha eneo hilo sasa kuwa na hati halali ya umiliki.

 

Katika kutekeleza agizo hilo, Mhe. Mmuya amekabidhi hati ya umiliki wa eneo la Kituo cha Afya Chinongwe kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Mhe. Fadhily Mbwelei baada ya eneo hilo kukamilisha taratibu za upimaji na uandaaji wa hati.

 

Amesema umiliki wa maeneo ya Serikali kwa hati ni hatua muhimu ya kulinda mali za umma na kuzuia migogoro ya ardhi, huku akisisitiza kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa wana wajibu wa kuhakikisha maeneo yote ya Serikali na taasisi zake yanatambulika na kumilikiwa kwa mujibu wa sheria.