Habari
MMUYA AWATAKA ARIMO KUONGEZA BIDII, USHIRIKIANO NA UWAZI
- 07 Sep, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka watumishi wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kufanya kazi kwa bidii, kuongeza ushirikiano na kuzingatia uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuchochea maendeleo endelevu ya chuo hicho na kuongeza mchango wake katika sekta ya ardhi nchini.
Mhe. Mmuya ameyasema hayo leo Septemba 5, 2026, wakati wa kikao na watumishi wa ARIMO mkoani Morogoro, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Agosti 30, 2026 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ya kufika chuoni hapo kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi na taasisi hiyo.
Amesema ARIMO ni taasisi muhimu katika kuandaa wataalamu wa sekta ya ardhi, hivyo ni lazima watumishi wake kutekeleza majukumu kwa kujituma, kushirikiana na kuwa wazi katika shughuli za chuo ili kuweka msingi imara wa maendeleo yake na kuhakikisha kinazalisha wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya Taifa.
Mhe. Mmuya pia amewataka watumishi kuendelea kujiendeleza kielimu na kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sekta, huku akiwapongeza kwa kazi wanayoifanya ya kuwaandaa wataalamu wa kada mbalimbali za ardhi.
Katika kikao hicho, wakufunzi wa ARIMO wameiomba Wizara kusimamia kwa karibu uandaaji na uboreshaji wa mitaala ya kada za ardhi ili iendane na mahitaji halisi ya sekta na soko la ajira. Wamesema baadhi ya wahitimu wamekuwa wakimaliza masomo lakini kushindwa kupata ajira, hali ambayo wameeleza inaweza kuchangiwa na mitaala kutokidhi kikamilifu mahitaji ya sekta na waajiri.
Wakufunzi hao pia wameiomba Wizara kuwawezesha kupata mafunzo ya kuwaendeleza kitaaluma, wakisema wakipatiwa fursa hiyo wataongeza uwezo wao na kuwa mabalozi wazuri wa kutekeleza ndoto na matarajio ya sekta ya ardhi nchini.
Aidha, watumishi hao wamewasilisha changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo, ikiwemo uhitaji wa kuboresha miundombinu na kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia, hususani kwa mafunzo ya vitendo ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hasa matumizi ya mifumo na Akili Mnemba (AI).
Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kwa sasa inaendelea kutoa mafunzo katika fani zikiwemo Jiomatikia, Mipango Miji na Mikoa, GIS pamoja na Usimamizi wa Ardhi, Uthamini na Usajili.