Habari

MMUYA AWAPA NGUVU WANAWAKE: “SIMAMENI IMARA, MILIKINI ARDHI”

  • 13 Aug, 2026
MMUYA AWAPA NGUVU WANAWAKE: “SIMAMENI IMARA, MILIKINI ARDHI”

Serikali imewataka wanawake nchini kusimama imara na kutumia fursa zilizopo kisheria kupata, kumiliki na kutumia ardhi kwa usalama, ikisema umiliki salama wa ardhi ni msingi muhimu wa uwezeshaji wa wanawake, ustawi wa familia na maendeleo ya jamii.

 

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 12, 2026, na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, wakati akizungumza katika Kongamano la Kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke (Stand for Her Land)” linalofanyika jijini Dodoma.

 

Mhe. Mmuya amesema ardhi si rasilimali ya kiuchumi pekee, bali ni msingi wa maisha, maendeleo, usalama wa familia na ustawi wa jamii, hivyo wanawake wanapaswa kuwa na nafasi sawa katika umiliki na kufanya maamuzi kuhusu ardhi.

 

Amesema Serikali imeweka misingi ya kisheria inayolinda haki za wanawake katika masuala ya ardhi kupitia Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114, akisisitiza kuwa hakuna mila, desturi au taratibu zinazopaswa kutumika kumnyima mwanamke haki yake ya kumiliki, kutumia na kunufaika na ardhi kwa mujibu wa sheria.

 

Ameongeza kuwa mwanamke mwenye ardhi salama anaweza kuitumia kwa shughuli za kilimo, biashara na uwekezaji, pamoja na kuitumia kama dhamana ya kupata mikopo pale inapokubalika kisheria, kujenga nyumba na kuweka msingi bora wa maisha ya familia.

 

Aidha, Mhe. Mmuya amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa, viongozi wa vijiji, viongozi wa kimila na wadau wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu ardhi, huku akiwataka wanawake kuongeza uelewa kuhusu haki zao na taratibu za kisheria za kulinda milki zao.

 

Kongamano hilo la Kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke” limewakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa ardhi, wadau wa maendeleo na viongozi wa wanawake, likiwa na kauli mbiu isemayo “Imarisha Haki na Milki Salama za Ardhi na Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi kupitia Uongozi wa Wanawake wa Ngazi ya Jamii.”