Habari
MMUYA AWAONYA WANANCHI KUACHA KUWEKA LAMINATION KWENYE HATI ZA ARDHI
- 22 Jul, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ametoa wito kwa wananchi nchini kuacha kuweka “lamination” kwenye hati za umiliki wa ardhi, akieleza kuwa kitendo hicho kinaweza kuleta changamoto katika uhakiki na matumizi ya nyaraka hizo.
Akitoa elimu kwa wananchi, Mhe. Mmuya amesisitiza kuwa hati ya umiliki wa ardhi ni nyaraka muhimu ya kisheria inayopaswa kuhifadhiwa kwa uangalifu bila kuwekwa “lamination”, ili kulinda ubora wake na kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kuhakiki au kufanya marekebisho ya taarifa zilizomo kwenye hati.
Mhe. Mmuya ametoa rai hiyo Julai 21, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Kliniki ya Ardhi iliyofanyika katika Ofisi ya Kata ya Peramiho B, Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.
Aidha, Naibu Waziri amewahimiza wananchi kuhakikisha wanapata hati za umiliki wa ardhi, akisisitiza kuwa hati ndiyo uthibitisho wa kisheria wa umiliki wa ardhi na kinga muhimu dhidi ya migogoro.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kuheshimu mipaka ya maeneo yanayomilikiwa kisheria na kuepuka kuingia katika maeneo ya wawekezaji au watu wengine bila kufuata taratibu za sheria, akibainisha kuwa kufanya hivyo kunaweza kutafsiriwa kama uvamizi wa ardhi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Wilman Kapenjama Ndile, amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la upimaji wa ardhi ili kutambua mipaka halali ya maeneo yao na kupunguza migogoro ya ardhi.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Juma Kijiji, amesema Kliniki ya Ardhi imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria, taratibu na huduma mbalimbali za sekta ya ardhi, hatua inayotarajiwa kuongeza uelewa na kupunguza migogoro inayotokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu masuala ya ardhi.
Katika Kliniki hii Jumla ya hati 225 zimeandaliwa na kukabidhiwa kwa wananchi, migogoro 14 ikipokelewa na takribani wananchi 527 wamehudumia tangu tarehe 14 – 21 Julai 2026.