Habari
MMUYA ATAKA WAMILIKI WA ARDHI KULIPA KODI YA PANGO LA ARDHI KWA WAKATI KUEPUKA RIBA YA ASILIMIA 1
- 21 Jun, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ametoa wito kwa wamiliki wote wa ardhi nchini kuhakikisha wanalipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wakati ili kuepukana na faini na adhabu zisizo za lazima.
Akizungumza leo, tarehe 20 Juni 2026, katika kikao kazi kilichowakutanisha wananchi wa Wilaya ya Arusha pamoja na wataalamu wa ardhi wa Mkoa wa Arusha kwenye Ukumbi wa Hazina Ndogo, Mhe. Mmuya amesisitiza kuwa serikali haitafanya mzaha na mtu yeyote atakayekiuka matakwa ya sheria hiyo.
Mhe. Mmuya ameweka wazi kuwa kila Mtanzania anayemiliki ardhi kihalali ana wajibu wa kisheria kulipa Kodi ya Pango la Ardhi. Aidha, amewaonya wale wanaotumia kisingizio cha kutofahamu sheria ili kukwepa wajibu huo.
"Kutokufahamu si kinga ya kutoadhibiwa. Sheria zetu zimeweka kipengele hiki wazi, na ukienda kinyume unaonekana ni mzembe tu. Sitaki niwaingize kwenye eneo hilo la kusema hamkufahamu," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.
Naibu Waziri amefafanua utaratibu wa ulipaji wa kodi hiyo kwa mwaka wa fedha, akibainisha kuwa wamiliki wote wa ardhi wanatakiwa kulipa kodi zao ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha bila kuongezewa riba au faini yoyote.
Hata hivyo, mmiliki yeyote ambaye atakuwa hajalipa kodi yake baada ya kipindi hicho ataingia rasmi katika hatua ya kutozwa penalti, ambapo atakatwa riba ya asilimia moja (1%) kila mwezi kulingana na kiasi anachodaiwa.
Ili kuondoa malalamiko na mkanganyiko miongoni mwa wananchi, Mhe. Mmuya amebainisha kuwa vigezo vitatu vikuu vinavyotumika kupanga viwango vya Kodi ya Pango la Ardhi ni ukubwa wa eneo, matumizi ya ardhi pamoja na eneo ilipo ardhi husika (location).