Habari
MMUYA APIGA MARUFUKU UVAMIZI WA MAENEO YA WAZI
- 22 Jun, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amepiga marufuku tabia ya uvamizi na ubadilishaji wa matumizi ya maeneo ya wazi kinyume cha sheria, akisisitiza kuwa serikali haitafanya msamaha kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu hizo.
Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo alipokutana na wananchi wa Wilaya ya Arusha pamoja na wataalamu wa ardhi wa Mkoa wa Arusha katika kikao kazi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina Ndogo jijini humo.
Akizungumza kwa msisitizo katika kikao hicho, Naibu Waziri amewataka wananchi na mamlaka husika kuwa walinzi wa maeneo ya wazi kama vile viwanja vya michezo na maeneo ya kupumzikia, ambayo yamepangwa kisheria kwa ajili ya kuboresha mandhari na ikolojia ya jiji.
"Hatupendi kuona maeneo ya wazi yanabadilishwa matumizi kwa kutokufuata utaratibu. Sisi tukija kugundua kama wenye dhamana, lazima tutatoa maelekezo eneo hilo libomolewe, libaki kwenye ardhi yake iliyopangwa na kuidhinishwa na wizara," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mmuya amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu endelevu na ya kutosha kwa wananchi kuhusu ulinzi na umuhimu wa maeneo ya wazi ili kuzuia migogoro na uharibifu kabla haujafanyika. Alibainisha kuwa elimu itasaidia jamii kuelewa wajibu wao na athari za kisheria za kuvamia ardhi ya umma.
"Ni muhimu kutoa elimu ya kutosha juu ya kulinda maeneo ya wazi. Hautakiwi hata siku moja kwenda kufanya maendelezo yoyote ya maeneo ya wazi bila kupata kibali cha mmiliki wa maeneo ya wazi ambaye ni mkurugenzi wa eneo lile," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.
Mhe. Mmuya amefafanua kuwa mamlaka ya kubadilisha matumizi ya ardhi si ya mtu binafsi wala maafisa wa chini, bali ni mchakato wa kisheria unaoanzia kwa mkurugenzi wa halmashauri na kushirikisha wananchi kupitia matangazo ya umma kwa muda wa mwezi mzima ili kutoa fursa ya maoni au mapingamizi.
"Wala sio Wizara ya Ardhi, wala sio Kamishna wa Ardhi, hairuhusiwi! Anayeomba kubadilisha matumizi ya eneo la ardhi ni yule aliyepanga. Wewe mwenyewe Mkurugenzi na watu wako, mnakaa kikao, mnajadili, mnakwenda kuweka tangazo kwenye lile eneo tangazo linakaa mwezi mzima kuwataka watu wote wenye maoni tofauti waseme," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.
Vilevile, Naibu Waziri amewaagiza wataalamu wa ardhi na wakurugenzi wa halmashauri kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara (regular monitoring) katika kila mtaa, kitongoji, na kijiji ili kubaini kama maendelezo yanayofanyika yanaendana na mipango miji iliyopangwa.
Aidha, ametoa agizo kwa wakurugenzi kuhakikisha maeneo yote ya wazi, shule, na hospitali yanapimwa na kupewa hati miliki ili kulinda maeneo hayo kisheria dhidi ya wavamizi.
"Eneo la wazi halimilikiwi na Wizara ya Ardhi, linamilikiwa na mkurugenzi wa eneo husika. Tena sasa hivi tumesema kabisa mpe na hati! Hata kwenye shule, hospitali toeni hati watu wakae na hati zao ili mkurugenzi ajue anamiliki kisheria," alisema Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya.