Habari
MMUYA APIGA MARUFUKU UANDAAJI WA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI KWENYE VIWANJA VYA MITA 20 KWA 20
- 29 Oct, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka wataalamu wa mipango miji nchini kuacha kuidhinisha mipango ya matumizi ya ardhi kwenye viwanja vyenye ukubwa wa mita 20 kwa 20, isipokuwa katika maeneo ambayo tayari yameendelezwa kupitia urasimishaji.
Mhe. Mmuya ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 28, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Wataalamu wa Mipango Miji uliofanyika jijini Arusha.
Amesema utaratibu huo unaweza kutumika katika maeneo ambayo tayari yameendelezwa na kufanyiwa urasimishaji, lakini si katika maeneo ambayo bado hayajaendelezwa.
Aidha, Mhe. Mmuya amewataka wataalamu wa mipango miji kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na uadilifu, akibainisha kuwa baadhi ya wataalamu wasio waadilifu wamekuwa wakinunua viwanja na kuandaa michoro isiyo halisi ambayo haitambuliki katika mifumo ya Wizara.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji, Bi. Martha Mkupasi, amesema Bodi hiyo itaendelea kuhakikisha taaluma ya mipango miji inachangia mabadiliko chanya katika ukuaji na maendeleo ya miji, kulinda maslahi ya umma na kusimamia maadili ya kitaaluma.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Bodi hiyo imewafutia usajili wataalamu wa mipango miji 36 pamoja na kampuni 15 kutokana na sababu za kimaadili.
Naye Rais wa Chama cha Maafisa wa Mipango Miji, Dkt. Juma Matindama, amesema jukumu kuu la Chama hicho ni kuendeleza taaluma ya mipango miji nchini.
Mkutano huo unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Mabadiliko ya Kidijitali katika Mipango Miji kwa Udhibiti Bora wa Ukuaji wa Miji.” Unalenga kujifunza, kubadilishana uzoefu, kutathmini hali ya mipango miji nchini na kuweka mikakati ya kuboresha maeneo yenye upungufu.