Habari

MMUYA AAGIZA KASI YA UTOAJI HUDUMA SEKTA YA ARDHI

  • 10 Aug, 2026
MMUYA AAGIZA KASI YA UTOAJI HUDUMA SEKTA YA ARDHI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka watumishi wa Wizara kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi huku akisisitiza kuwa kila Mtanzania mwenye sifa na vielelezo halali vya kupatiwa hati milki ya Ardhi anapaswa kupata hati yake kwa wakati.

 

Mhe. Mmuya ameyasema hayo leo, Agosti 8, 2026, alipotembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, ambapo amewataka watumishi kujivunia kazi wanayoifanya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka na kwa ufanisi.

 

Amesisitiza kuwa Wizara ya Ardhi ni Wizara ya kuwasaidia wananchi na siyo Wizara ya migogoro. “Kila mtumishi ajisikie furaha na amani kufanya kazi Wizara ya Ardhi,” amesema.

 

Aidha, Mhe. Mmuya ameagiza kufanyika kwa uhakiki wa haraka wa nyaraka za wananchi ili wale wenye sifa wapate hati zao bila kuchelewa, huku akitaka kuwepo utaratibu wa kuwafuatilia Watanzania wanaostahili hati lakini bado hawajazipata. “Tuhakikishe kila mwenye sifa anapata hati yake kwa wakati,” amesema.

 

Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Bi. Happiness Mtutwa, amesema jumla ya maombi 1,200 ya hati yamepokelewa katika kipindi cha Maonesho ya Nane Nane, ambapo maombi 1,152 tayari yameshasajiliwa, jambo alilolieleza kuwa, linaonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupata huduma za ardhi.

 

Naye mmoja wa mwananchi aliyefika bandani hapo kupatiwa hati yake Ndugu Emmanuel Miselya amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika Banda la Wizara ya Ardhi akieleza kuwa huduma zinapatikana na wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kupata hati za ardhi kwa wakati.

 

Akihitimisha, Mhe. Mmuya amewataka wananchi kuepuka kuzikabidhi hati zao za ardhi kwa watu wasio waaminifu au kuzitumia katika mazingira yasiyo sahihi, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha changamoto za kisheria na kifedha. 

 

Aidha, amewataka wadau kuendelea kushirikiana na Wizara katika kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza imani ya wananchi katika huduma za ardhi.