Habari

MIRADI 21 KUIMARISHA MAKAZI KARIAKOO

  • 30 Jan, 2024
MIRADI 21 KUIMARISHA MAKAZI KARIAKOO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ameshuhudia utiaji saini wa mikataba 21 ya Ubia kati ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Sekta binafsi utakaotatua changamoto za majengo chakavu na kujenga mapya ili kubadili sura ya eneo la kariakoo na kuwa ya Kisasa.

 

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini iliyofanyika katika Jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es salaam Waziri wa Ardhi Silaa amesema Shirika limesaini mikataba na wabia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 21 ambayo ina thamani ya zaidi bilioni 271 ikilinganishwa na thamani ya sasa ya majengo hayo ambayo ni bilioni 59.

 

Waziri Silaa ameongeza kuwa endapo miradi  hiyo itakamilika kwa wakati kama masharti ya mkataba husika utasaidia kutatua changamoto za makazi bora na maeneo ya biashara na kubadili sura ya Soko la kariakoo na kuwa ya Kisasa.

 

Aidha, Waziri Silaa amebainisha kuwa miradi hiyo itakuwa na wapangaji 2,011 ambapo wapangaji 1,258 ni wa maduka na 500 ni stoo  huku 255 wa wapangaji wa  nyumba za makazi  ikilinganishwa na idadi ya wapangaji ya sasa ambayo ni 190 kati yao wapangaji wa maduka ni 118 na nyumba za makazi ni 72 

 

Kadhalika Waziri Silaa amelitahadharisha Shirika hilo Kuwachuja wabia kwa umakini ili kuweza kupata waendelezaji makini na wenye uwezo wa kukamilisha miradi kwa wakati.

 

Ifahamike sera ya Ubia inalenga kuleta mazingira bora ya kibiashara, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya Umma, ambapo Sera ya kwanza ya Ubia ilipitishwa mwaka 1993 na kufanyiwa marekebisho kadhaa katika miaka ya 1998, 2006 na 2012.