Habari

MIGOGORO YA ARDHI ITATULIWE KABLA YA URASIMISHAJI KUANZA

  • 28 Jun, 2024
MIGOGORO YA ARDHI ITATULIWE KABLA YA URASIMISHAJI KUANZA

Serikali imewaagiza viongozi katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kumaliza migogoro ya mipaka, matumizi ya ardhi na umiliki wa ardhi baina yao mapema ili kuharakisha utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) pindi utakapoanza utekelezaji.

 

Agizo hilo limetolewa tarehe 28 Juni 2028 na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bw. Said Kitinga wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

 

Amesema, kila kiongozi katika eneo lake atoe elimu sahihi kwa wananchi juu ya utekelezaji wa mradi huo ili utekelezwe kwa ufanisi na kutimiza lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa watanzania.

 

‘‘Katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga takribani Viwanja 40,474 vitatambuliwa, vitapangwa, vitapimwa na kumilikishwa kwa wananchi katika maeneo yatakayofikiwa na mradi pamoja na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi, kutoa elimu ya masuala ya ardhi pamoja na kutoa hamasa juu ya usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi’’ amesema Mtatiro

 

Ameongeza kuwa, Utekelezaji mradi huo utahusisha utambuzi wa kila kipande cha ardhi, Upangaji wa maeneo yote yaliyotambuliwa kwa kuandaa michoro ya mipangomiji, Upimaji wa viwanja vilivyopangwa kwa kuweka alama za upimaji na kuandaa ramani za upimaji na wananchi kumilikishwa maeneo yao kwa kupewa Hatimilki. 

 

Mwakilishi wa Makundi Maalum Bw. Isaack Timothy amesema kuwa, wamepata elimu ya masuala ya ardhi na namna mradi utatekelezwa katika wilaya yao na kukiri kuwa wamefurahi kuona namna ambavyo makundi maalum yamepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huu.

 

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) umedhamira kumaliza changamoto ya makazi holela kwa kuyafikia maeneo ambayo yameendelezwa bila kupangwa na hayajafikiwa na zoezi la urasimishaji katika Halmashauri zipatazo 60 nchini.