Habari
MHANDISI SANGA AKAGUA ENEO LA SAMIA ARUSHA AFCON CITY
- 29 Aug, 2024
Katibu Mkuu wzara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amekakagua eneo la Mradi wa Samia Arusha AFCON City (SAAC).
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 4,555.5 lipo Kata ya Olmot na Olasiti katika Jiji la Arusha na limepakana na miradi miwili ya viwanja vitakavyotumika kwenye mashindano ya Afcon 2027.
Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa miguu ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika mwaka 2027 ambapo tayari eneo litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa michezo hiyo limebanishwa.
Mhandisi Sanga ametembelea eneo hilo tarehe 28 Agosti 2024 jijini Arusha ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha mradi uliopangwa kutekelezwa kwenye eneo hilo unatekelezwa kwa wakati ambapo Wizara yake imelekeza eneo hilo kupangwa, kupimwa na kumilikishwa.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Arusha Geofrey Mwamsojo, eneo hilo likipangwa litawekwa huduma muhimu zitakazowezesha kuwa na mji nadhifu kulingana na matumizi yanayoendana na matumizi ya uwanja.
Amesema, Malengo ya mradi huo ni kuwa na mji nadhifu na himilifu na unaojitegemea wenye huduma zote wezeshi kwa uwanja wa michezo, kusaidia maendeleo ya Jiji la Arusha yanayofuata mpangilio bora wa makazi pamoja na kuongeza wigo wa viwanja vitakavyojengwa Hotel za kitalii kwa ajili ya Jiji la Arusha.
Mradi huo wa Samia Arusha Afcon City utatekelezwa kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza ni utwaaji vipande vya ardhi pamoja na uthamini wa fidia ya vipande vya ardhi vitakavyoguswa na mradi, awamu ya pili kupanga eneo zima la mradi lenye ukubwa wa ekari 4555.5, Kupima eneo lenye ukubwa wa ekari 180 ili kugawa viwanja pamoja na Kufungua miundombinu ya barabara kuu na za ndani.
Awamu ya mwisho itakuwa endelevu na kuhusisha kazi za umilikishaji wa viwanja, maandalizi ya hati na vikao vya kamati ya ugawaji wa ardhi pamoja na usimamizi wa mradi utakao husisha utangazaji wa uuzaji wa viwanja vya mradi.