Habari

MFUMO WA KIELEKTRONIKI WAJA KUHARAKISHA MAAMUZI YA MASHAURI YA ARDHI KWA HAKI NA KWA WAKATI 

  • 23 May, 2024
MFUMO WA KIELEKTRONIKI WAJA KUHARAKISHA MAAMUZI YA MASHAURI YA ARDHI KWA HAKI NA KWA WAKATI 

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaanzisha mfumo wa Kieletroniki maarufu Integrated Land Cases Management System - ILCMS utakaotumiwa na Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya kwa lengo la kuharakisha na kuondoa mlundikano wa mashauri ya ardhi katika Mabaraza hayo. 

 

Wenyeviti na Wasajili wasaidizi wa Kanda wa Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya wanakutana Jijijini Arusha katika kikao kazi pamoja na masuala mengine kujifunza na namna bora ya kutumia mfumo wa ILCMS mfumo unaolenga kupunguza mlundikano wa mashauri na kutoa haki kwa wakati.

 

Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Eng. Anthony Sanga, Mkurugenzi wa Utwala na Rasmali Watu Bw. Sheushi Mbuli aliwaambia Wenyeviti na Wasajili wa Mbaraza hayo kuwa mfumo huo unalenga kurahisha usajili, usikilizwaji na umalizaji wa mashauri ya ardhi kwa haki na kwa wakati. 

 

Kiongozi huyo wa Wizara ya Ardhi alibainisha kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 3 (1) (m) cha Sheria ya Ardhi Sura ya 113 kinaeleza msingi mmojawapo wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, ni kuhakikisha mashauri ya ardhi yanaamuliwa kwa wakati.

 

‘’Mfumo huu unamwezesha mdaiwa na Mawakili kufungua shauri lake, kulipia, kuwasilisha nyaraka zinazohusiana na shauri hilo, pamoja na kupata taarifa za shauri lake kama vile wito na kuahirishwa kwa mashauri akiwa popote bila kulazimika kufika katika Baraza husika.’’Aliongeza Bw. Mbuli

 

Bw. Mbuli alitaja faida za mfumo huo kuwa ni kurahisisha ufunguzi wa kesi , kusajili na malipo ya shauri husika kwa wakati, kupata taarifa za mashauri yao pasipo kwenda Ofisi za Mabaraza husika na kusaidia uwasilishaji wa nyaraka zinazohusiana na shauri husika kwa usalama, haraka na uhakika.

 

Faida nyingine ni kwamba mfumo utampunguzia Mwenyekiti safari za kutembelea maeneo yenye migogoro ya mara kwa mara endapo taarifa zitajazwa kwa usahihi na kupunguza msongamano wa watu katika Baraza na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma.

 

Aidha Mfumo huo pia utasaidia wananchi kupata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji badala ya kutumia muda mwingi kwenda Mahakamani, utawapunguzia wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu kufata Baraza kwa huduma.

 

Wasajili wa Mabaraza pamoja na Wenyeviti kote Nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili watakaporudi katika vituo vyao vya kazi wawe tayari kuanza kutumia mfumo katika utekelezaji wa majukumu yao.