Habari

MFUMO WA e-Ardhi: MWANANCHI KUOMBA NA KUSAINI HATI MILKI YA ARDHI MKOA WOWOTE ALIPO

  • 18 Sep, 2026
MFUMO WA e-Ardhi: MWANANCHI KUOMBA NA KUSAINI HATI MILKI YA ARDHI MKOA WOWOTE ALIPO

Wananchi nchini sasa wanaweza kupata na kukamilisha baadhi ya huduma za ardhi kwa urahisi zaidi kupitia mfumo wa kidijiti wa e-Ardhi, ikiwemo kusaini hati zao bila kulazimika kusafiri hadi mkoa ambako huduma ilianzishwa.

 

Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya mfumo wa e-Ardhi kupitia Jogoo FM Ruvuma, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Juma Kijiji, amesema mfumo huo umeleta maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za ardhi kwa kutumia teknolojia.

 

Amesema, miongoni mwa manufaa ya mfumo huo ni kumwezesha mwananchi kupata huduma kwa urahisi, kupunguza gharama na muda wa kusafiri, pamoja na kurahisisha ufuatiliaji wa huduma za ardhi.

 

“Kupitia mfumo wa e-Ardhi, mwananchi anaweza kusaini hati yake akiwa mkoa wowote alipo, hivyo si lazima kusafiri kwenda mkoa ambako huduma yake ilianzishwa,” amesema Bw. Kijiji.

 

Kwa upande wake, Afisa Ardhi Mwandamizi kutoka Makao Makuu, Bw. Hisani Mtolera,amewataka wananchi na wadau wa sekta ya ardhi kujifunza na kutumia mfumo wa e-Ardhi ili kunufaika na huduma zinazotolewa kwa njia ya kidijiti.

 

Amesema matumizi ya mfumo huo yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya maboresho ya huduma za ardhi, kwa kuwezesha wananchi kupata huduma kwa ufanisi na kwa urahisi zaidi.

 

Naye Msajili wa Hati Msaidizi Mkoa wa Ruvuma, Bi. Christina Nyerere   ametoa wito kwa wananchi kuupokea mfumo,kuutumia na kuendelea kujenga uelewa kuhusu mfumo wa e-Ardhi na kutumia fursa hiyo kufuatilia na kupata huduma za ardhi kwa njia ya kidijiti.

 

Elimu hiyo kwa umma imetolewa kupitia Jogoo FM Ruvuma ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali, kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, za kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijiti katika upatikanaji wa huduma za ardhi.