Habari
MFUMO WA e-ARDHI MTWARA WAFANYA MAPINDUZI MAKUBWA: MASIJALA ZA ARDHI ZENYE MAJARIDA SASA ZAHAMIA KIDIJITI
- 22 Sep, 2026
Mkoa wa Mtwara umeanza kushuhudia mabadiliko makubwa katika usimamizi na uhifadhi wa taarifa za ardhi kupitia Mfumo wa e-Ardhi, ambapo masijala za ardhi zilizokuwa zikihifadhiwa kwa kutumia majarida sasa taarifa hizo zinaendelea kuhamishiwa katika mfumo wa kidijiti.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha huduma za ardhi kwa kutumia teknolojia, huku ikilenga kuimarisha usalama wa taarifa za wananchi, kupunguza utegemezi wa nyaraka za karatasi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za ardhi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumzia hatua hiyo, Afisa Kumbukumbu kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Bw. Mark Mtokambali, amesema uhamishaji wa taarifa kutoka katika majarida kwenda kwenye mfumo wa kidijiti utasaidia kuimarisha uhifadhi na usalama wa taarifa za ardhi za wananchi.
Kwa upande wao, Maafisa Ardhi Wasaidizi, Bi. Maimuna Badi na Bi. Generose James, wamepongeza juhudi hizo za Serikali, wakieleza kuwa mfumo wa e-Ardhi utarahisisha usimamizi wa taarifa, kupunguza changamoto za upotevu au uharibifu wa majalada na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.