Habari
MFUMO WA e-ARDHI KUSAIDIA KUTUNZA KUMBUKUMBU ZA ARDHI NCHINI
- 20 Aug, 2024
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imepokea na kujadili taarifa ya Utekelezaji wa Usimikaji wa Mfumo wa Unganishi wa Taarifa za Ardhi unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Najma Giga amesema ni vema Mfumo huo ukamilishwe kwa wakati ili kuhakikisha kunakuwa na taarifa na kutunza kumbukumbu sahihi za ardhi nchi nzima.
Awali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Degratius Ndejembi amewahakikishia wajumbe wa Kamati hiyo ushirikiano wa hali na mali ili kufikia azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ardhi yote nchini inakuwa salama kwa kuwa na Kumbukumbu sahihi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amesema Mfumo huo unalenga kuongeza mapato ya Serikali na kuongeza uwazi na kuleta thank ya uwajibikaji kwa watumishi wa sekta ya Ardhi.
Aidha, wajumbe wa Kamati hiyo wamepata semina kuhusu Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la 2023 ambayo imepitishwa rasmi na Baraza la Mawaziri Agosti 18, 2023 ili kuhakikisha kuna usawa katika upatikanaji wa Ardhi, usimamizi na matumizi ya ardhi kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera.