Habari

MFUMO WA e-ARDHI KUKAMILIKA IFIKAPO JUNI 2026

  • 21 Jan, 2025
MFUMO WA e-ARDHI KUKAMILIKA IFIKAPO JUNI 2026

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kukamilisha Mfumo wa e-Ardhi na kuanza kutumika katika halmashauri 20 nchini.

Mhe. Timotheo Mzava ametoa pongezi hizo Januari 21, 2025 jijini Dodoma wakati Kamati hiyo inapokea na kujadili taarifa ya utekelezaji na hatua iliyofikiwa katika ujenzi na usambazaji na matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi nchini.

"Mfumo huu ni suluhisho la changamoto ya ardhi nchini, utapunguza sana migogoro ya ardhi. Wataalamu waangalie namna ya kutatua changamoto zinazojitokeza na mradi huu wa TEHAMA ukamilike kwa wakati kwa nchi nzima" amesema Mhe. Mzava.

Mhe. Mzava amesema ipo migogoro mingi ya ardhi lakini panapokuwa na mfumo, migogoro itapungua kwa kuwa huduma zitatolewa kupitia mfumo wa e-Ardhi na ameitaka wizara kuangalia namna ya kutatua changamoto zilizojitokeza kutokana na matumizi ya mfumo.

Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema changamoto zilizojitokeza wakati wa matumizi ya mfumo wa e-Ardhi zinaendelea kushughulikiwa hatua itakayofanya mfumo huo kuwa na ufanisi zaidi.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Geophrey Pinda, Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Wizarani hapo Bw. Flateny Michael Hassan amesema mfumo wa e-Ardhi katika utekelezaji wa bajeti ya 2024/2025 umefikia halmashauri 20 ikiwemo jiji la Arusha, Dodoma na mfumo huo unatarajiwa kukamilika na kutumika katika halmashauri zote za Tanzania Bara kufikia Juni 2026.

Akielezea zaidi kuhusu mfumo huo Bw. Flateny amesema, lengo kubwa la mfumo wa e-Ardhi ni kuboresha huduma za sekta ya ardhi hasa katika urahishaji na usajili wa hati na nyaraka kwa kuwa hakutakuwa na matumizi ya karatasi na kila kitu kitafanyika kupitia mfumo na kuongeza mapato ya Serikali.

Bw. Flateny ameongeza kuwa matumizi ya mfumo huo wa e-Ardhi utapunguza muda na gharama kwa kuwa mwananchi hatalazimika tena kusafiri ili kupata huduma