Habari

MBUNGE SINGIDA MJINI AIPONGEZA WIZARA YA ARDHI KWA KUANZISHA SAMIA ARDHI KLINIKI ILI KUWAINUA WANAWAKE

  • 04 Mar, 2026
MBUNGE SINGIDA MJINI AIPONGEZA WIZARA YA ARDHI KWA KUANZISHA SAMIA ARDHI KLINIKI ILI KUWAINUA WANAWAKE

Mbunge wa Singida Mjini, Yagi Kiaratu, ameipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuanzisha programu ya Samia Ardhi Kliniki, akisema kuwa imeleta manufaa makubwa kwa wanawake mkoani Singida.

 

Mheshimiwa Kiaratu ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea Banda la Ardhi lililokuwa likitoa huduma na elimu kwa wananchi wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika mkoani Singida.

 

 Amesema kliniki hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kuwasaidia wanawake kupata elimu ya umiliki wa ardhi, usajili wa hati, pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

 

“Nawapongeza sana Kamishna na Wizara kwa kuanzisha,Samia Ardhi Kliniki kwaani inawafikia wanawake moja kwa moja na kuwapa uelewa wa haki zao za kumiliki ardhi. Hii ni hatua kubwa katika kuwawezesha kiuchumi na kijamii,” amesema Mheshimiwa Kiaratu.

 

Aidha, amebainisha kuwa wanawake wengi wamejitokeza kupata huduma na ushauri wa kitaalamu, jambo linaloonesha mwitikio chanya wa jamii kuhusu masuala ya ardhi. 

 

Amehimiza juhudi hizi ziendelezwe ili kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanapata hati miliki na kulinda rasilimali zao kwa manufaa ya familia na taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Bi Shamim Hoza amesema wanaendelea kutoa elimu na huduma rafiki kwa wananchi, hasa wanawake, ili kuhakikisha wanapata haki na usalama wa milki zao.

 

Kongamano hilo limeendelea kuwa chachu ya kuhamasisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia umiliki salama wa ardhi.