Habari
MAMLAKA ZA UPANGAJI ZATAKIWA KUEPUKA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI KWENYE MAENEO HATARISHI
- 30 Oct, 2026
Mamlaka za Upangaji nchini zimetakiwa kuepuka kuandaa na kuidhinisha mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo hatarishi, ikiwemo mabonde na maeneo yanayopitisha maji, ili kulinda usalama wa wananchi na kuimarisha usimamizi bora wa matumizi ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya amewasisitiza wataalamu wa hao kuzingatia hali halisi ya maeneo kabla ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kutambua maeneo yenye vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha maisha ya wananchi makazi yao na mali zao.
Mhe. Mmuya ametoa maelekezo hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Wataalamu wa Mipango Miji uliofanyika jijini Arusha, Oktoba 28, 2026, uliokuwa na kaulimbiu isemayo “Mabadiliko ya Kidijiti katika Mipangomiji kwa Udhibiti Bora wa Ukuaji wa Miji.”
Amesema upangaji bora wa matumizi ya ardhi ni hatua muhimu katika kuzuia wananchi kuanzisha makazi katika maeneo yasiyofaa kwa maendeleo ya makazi, huku akiwataka wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia maslahi mapana ya umma.
Aidha, Mhe. Mmuya amewataka wataalamu wa Mipangomiji kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhimiza tahadhari na ulinzi wa watu wakati wa El Nino kwa kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inazingatia usalama wa wananchi wote na mazingira yanayowazunguka.
Amesisitiza kuwa mamlaka za upangaji na wataalamu wa mipango miji wana wajibu wa kuhakikisha maamuzi ya upangaji yanazingatia usalama, ustawi wa wananchi na matumizi endelevu ya ardhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.