Habari

Mama Samia Legal Aid Yachanja Mbuga Dodoma: Wananchi Zaidi ya 40,000 Wanufaika, Kamishna wa Ardhi Apongeza Huduma za Nyumba kwa Nyumba

  • 12 May, 2026
Mama Samia Legal Aid Yachanja Mbuga Dodoma: Wananchi Zaidi ya 40,000 Wanufaika, Kamishna wa Ardhi Apongeza Huduma za Nyumba kwa Nyumba

Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea kuleta mafanikio makubwa mkoani Dodoma huku maelfu ya wananchi wakiendelea kufikiwa na huduma za msaada wa kisheria na elimu mbalimbali zinazolenga kuwasaidia kutambua haki zao na kupata huduma karibu yao.

 

Katika kuonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa ukaribu zaidi, Kamishna wa Ardhi nchini, Happiness Mututwa ametembelea maeneo ya Mpwapwa na Kibaigwa mkoani Dodoma kukagua maendeleo ya utekelezaji wa kampeni hiyo pamoja na kuzungumza na wananchi wanaonufaika na huduma hizo.

 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mututwa amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshiriki kikamilifu katika kampeni hiyo kwa kupeleka wataalamu wake katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja na kutatua changamoto zinazohusu ardhi, nyumba na makazi.

 

Amesema hatua ya wataalamu hao kupita nyumba hadi nyumba pamoja na kata hadi kata imesaidia wananchi wengi kupata huduma kwa urahisi zaidi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

 

“Tunawapongeza wataalamu wetu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwafuata wananchi majumbani mwao na kutoa huduma karibu yao. Hii ni hatua muhimu inayotekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote,” amesema Mututwa.

 

Aidha, Kamishna huyo wa Ardhi ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni hiyo ili waweze kunufaika na elimu ya msaada wa kisheria pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia wizara na taasisi zake.

 

Kwa upande wake, Afisa Utumishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni ya Mama Samia Legal Aid Awamu ya Pili katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Tiara Pambaiko amesema tangu kuanza kwa kampeni hiyo Mei Mosi mwaka 2026, zaidi ya wananchi 40,000 tayari wamefikiwa na elimu pamoja na huduma mbalimbali za msaada wa kisheria.

 

Amesema wananchi hao wamefikiwa kupitia njia tofauti ikiwemo wataalamu kwenda katika shule, kata, vijiji pamoja na maeneo wanayoishi wananchi kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kusikilizwa na kuhudumiwa.

 

Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea nchini kote ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata haki, elimu ya sheria na huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi zaidi.