Habari

MABARAZA YA ARDHI YANAMCHANGO KATIKA KUSULUHISHA MIGOGORO YA ARDHI

  • 29 Jan, 2024
MABARAZA YA ARDHI YANAMCHANGO KATIKA KUSULUHISHA MIGOGORO YA ARDHI

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba imeshiriki uzinduzi wa Wiki ya Sheria jijini Dodoma yakiongozwa na Mhe. Dkt. Tulia Ackson Spika wa Bunge la Tanzania.

 

Uzinduzi huo umefanyika Januari 27, 2024 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ukitanguliwa na matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria ambao umehusisha viongozi mbalimbali wa mahama, watumishi wa umma na wananchi kutoka jiji la Dodoma.

 

Akizungumzia ushiriki wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Dodoma Bw. Jackson Kanyerinyeri amesema kuwa moja ya jukumu lao ni kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda hilo katika masuala ya ardhi, migogoro ya ardhi namna inavyotatuliwa katika mabaraza hayo hadi kutolewa hukumu.

 

 

Bw. Kanyerinyeri ameongeza kuwa wamepata wasaa mujarabu wa kuwaeleza wananchi juu ya mabadiliko ya Sheria Na 3 ya 2021 ambayo imeondoa mamlaka ya mabaraza ya Kata kusikiliza kesi za migogoro ya ardhi badala yake mabaraza hayo yana jukumu la kusikiliza na kusuluhisha migogoro baina ya wananchi ikishindikana migogoro hiyo iwasilishwe Baraza la Ardhi na nyumba la wilaya na kupewa cheti ndani ya siku 30.

 

Aidha, Bw. Kanyerinyeri ameongeza kuwa wanaendelea kuwasistiza wananchi wamalize migogoro ya ardhi kwa nyia ya mazungumzo na mapatano hatua inayookoa muda, kuondoa uhasama na inawapa wananchi muda wa kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

 

Wiki ya Sheria 2024 imeanza Januari 24 na inatarajiwa kuhitimishwa Januari 30 yakiongozwa na kaulimbiu “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai”