Habari

KLINIKI ZA ARDHI ZALETA MATOKEO KIGOMA, MIGOGORO 1,046 YAPATIWA UFUMBUZI

  • 12 May, 2026
KLINIKI ZA ARDHI ZALETA MATOKEO KIGOMA, MIGOGORO 1,046 YAPATIWA UFUMBUZI

Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Kigoma inapungua na hatimaye kumalizika kabisa kupitia mikakati ya kisekta inayotekelezwa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali.

 

Kauli hiyo imetolewa mapema Bungeni leo tarehe 11 Mei 2026 na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando, aliyehoji kuhusu mikakati ya Serikali ya kumaliza migogoro mingi ya ardhi inayowakabili wananchi wa Kigoma Mjini.

 

Mhe. Mmuya amesema migogoro ya ardhi imekuwa ikiathiri wananchi wengi nchini ikiwemo Mkoa wa Kigoma kutokana na mwingiliano wa matumizi ya ardhi, uuzwaji wa ardhi usiozingatia sheria na mamlaka husika, uvamizi wa maeneo ya umma na mashamba makubwa pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya ardhi na mipaka ya kiutawala.

 

Amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imeendelea kutatua migogoro hiyo kupitia Ofisi za Makamishna wa Ardhi wa Mikoa, Kliniki za Ardhi zinazoendelea nchini pamoja na vikao na mikutano ya viongozi.

 

Mkoa wa Kigoma umefanya jumla ya Kliniki za Ardhi tano, huku katika mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya migogoro ya ardhi 1,092 ikipokelewa na kusikilizwa ambapo kati ya hiyo migogoro 1,046 ilitatuliwa. Migogoro 46 iliyobaki ipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.

 

Aidha, Naibu Waziri huyu amesema kuwa serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kuisimamia, kuendesha programu za Kliniki za Ardhi, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi ili kuzuia migogoro inayoweza kuzuilika pamoja na kuandaa rejista za migogoro kwa lengo la kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mashauri ya ardhi.

 

Sambamba na hilo Mhe. Kaspar Mmuya amesema serikali imeendelea kusisitiza kuimarishwa kwa nidhamu kwa watumishi wa Sekta ya Ardhi ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi katika kushughulikia changamoto za wananchi.