Habari
KLINIKI YA ARDHI LINDI KUTUMIKA KUSAJILI WANANCHI MATUMIZI YA MFUMO WA e-ARDHI
- 22 Sep, 2026
Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Lindi inatarajia kuendesha kliniki ya Ardhi kwa siku tano (kuanzia 23 Sept 2026 mpaka 27 sept 2026) katika Mtaa wa Mpilipili mkoani humo kwa lengo la kuendelea kuwasajili sambamba na kuwahudumia wananchi kupitia mfumo wa e-Ardhi.
Hayo yamebainishwa Leo tarehe 21 Septemba 2026 na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Lindi, Bw. Joffrey Martin wakati akihitimisha mafunzo ya siku nane ya mfumo wa e-Ardho yaliyolenga kuwajengea uwezo wataalam wa sekta ya ardhi mkoani humo kuhusu matumizi ya mfumo huo wa kidijitali.
Amewataka wananchi, taasisi za Serikali na makampuni kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo ili kupata huduma za ardhi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu kwa njia ya kidijiti.
Akigeukia mafunzo ya matumizi ya mfumo wa e-Ardhi kwa mkoa wake Bw. Martin amesema jumla ya michoro saba (7) ya mipango miji yenye jumla ya viwanja 4,322 imeingizwa katika mfumo, ambapo michoro sita (6) ni ya Manispaa ya Lindi na mmoja (1) ni wa Wilaya ya Kilwa.
Aidha, ameongeza kuwa, jumla ya hati saba (7) tayari zimetolewa kwa wananchi walioomba kupitia mfumo huo, baadhi yao wakipata hati ndani ya siku mbili tu.
"Mfumo wa e-Ardhi unatusaidia kuondoa utoaji hati miliki za karatasi na kuhamia kwenye hati za kielektroniki". Amesema
Kwa upande wao wananchi walionufaika na matumizi ya mfumo huo wamesema amefanikiwa kupata hati ndani ya siku mbili tangu walipowasilisha maombi.
"Nimekuja kuchukua hati ambayo niliomba ndani ya siku mbili, na ndani ya hizo siku mbili nimeipata. Mfumo huu ni rahisi sana ukilinganisha na wa zamani". Amesema Bi. Naombaelia Nasari,
Naye Bi. Khuda Ali Nalaga aliyefanikiwa kupata hati yake kupitia mfumo wa e-Ardhi, amewataka wananchi wengine kutumia mfumo huo kwa kuwa unapatikana kwa njia ya mtandao na mwananchi anaweza kuutumia hata akiwa nyumbani.
Mfumo wa e-Ardhi umeundwa kuwezesha huduma mbalimbali za ardhi kutolewa kwa njia ya kidijiti ikiwemo uwasilishaji na ufuatiliaji wa maombi, usimamizi wa taarifa za ardhi pamoja na kurahisisha upatikanaji huduma kwa wananchi.