Habari
KLINIKI YA ARDHI KIDIJITI YALETA NEEMA TABORA: HATI ZAIDI YA 200 ZATOLEWA TABORA MJINI NA NZEGA
- 29 Sep, 2026
Wananchi wa Mkoa wa Tabora wameendelea kunufaika na huduma zinazotolewa kupitia Kliniki ya Ardhi Kidijiti, ambapo jumla ya Hati Miliki za Ardhi zaidi ya 200 zimetolewa kwa wananchi wa Tabora Mjini na Wilaya ya Nzega, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi na kuwawezesha wananchi kutumia ardhi zao kama fursa ya maendeleo.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa Kliniki hiyo, Msajili wa Hati Msaidizi Mkoa wa Tabora, Bw. Samweli Ibrahimu, amesema hadi sasa jumla ya Hati Miliki zaidi ya 80 zimetolewa kwa wananchi wa Nzega, huku Hati 122 zikiwa zimetolewa katika Manispaa ya Tabora.
Amesema kasi hiyo ya utoaji wa hati inatarajiwa kuongezeka zaidi na kwamba hadi kufikia mwisho wa Kliniki ya Ardhi Kidijiti, Oktoba 3, 2026, zaidi ya hati 300 zinatarajiwa kuwa zimetolewa kwa wananchi.
“Utoaji wa hati hizi ni sehemu ya utekelezaji wa matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi, unaowezesha huduma za ardhi kutolewa kwa njia ya kidijiti kwa ufanisi, haraka na kwa uwazi zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, mwananchi aliyenufaika na huduma za Kliniki hiyo, Frednand Kornel Malenga ameishukuru Serikali kwa kuandaa kliniki hiyo, akisema imemrahisishia kupata huduma za ardhi bila usumbufu.
Amesema Kupitia Kliniki ya Ardhi Kidijiti, wananchi wa Tabora na Nzega wamepata fursa ya kufuatilia na kukamilisha huduma mbalimbali za ardhi, zikiwemo upatikanaji wa Hati Miliki, ushauri wa kitaalamu kuhusu umiliki wa ardhi, ufafanuzi wa changamoto za ardhi pamoja na elimu kuhusu matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za ardhi kupitia Mfumo wa e-Ardhi, ikiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata Huduma Bora, Haraka na Kidijitali.
e-Ardhi: Huduma popote. Hati yako, haki yako, maendeleo yako.