Habari

KLINIK YA ARDHI YAENDESHWA MTAA KWA MTAA ILEMELA

  • 09 Oct, 2024
KLINIK YA ARDHI YAENDESHWA MTAA KWA MTAA ILEMELA

Ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Mwanza imeendesha Klinik ya Ardhi katika halmashauri ya Ilemela mtaa kwa mtaa ili kuwafikia wananchi wengi kwa haraka na kuwapatia huduma za ardhi wanazohitaji katika maeneo yao.

 

"Kama mnavyofahamu tumekuwa na haya mazoezi ya Kliniki za Ardhi mara kadhaa, na kwa manispaa ya Ilemela tumeshaanza kwa ngazi ya mtaa kwa mtaa” amesema Happiness Mtutwa, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza

 

Akizungumza wakati wa Kliniki ya Ardhi iliyofanyika Oktoba 08, 2024 eneo la Nyasaka Ilemela mkoani Mwanza, Bi.Happiness ameweka wazi kuwa, Wizara ya Ardhi  inaendelea kutoa huduma za ardhi kupitia Kliniki za Ardhi alizoieleza kuwa  zimekuwa na mafanikio makubwa katika maeneo  mbalimbali nchini.

 

Kwa upande wake Dkt. Angelina Mabula, Mbunge wa jimbo la Ilemela Mkoani Mwanza amesema Kliniki ya Ardhi imeleta matokeo chanya kwa sababu imepunguza changamoto za ardhi na kuleta tija Zaidi kwa wananchi.

 

“Naomba Kliniki hizi ziendelee ili wananchi wapate huduma, lengo ni kuona kwamba ardhi inakuwa tena sio ardhi yenye changamoto, bali ni ardhi ya uwekezaji, mtu afaidike na ardhi yake, ardhi ni mali, ardhi ni mtaji ukiutumia vizuri utakunufaisha” amesema Dkt. Mabula.

 

Naye mzee Evarist Kabati Mkazi wa Kiseke jijini Mwanza amefurahishwa kwa kupata Hati ya kiwanja chake chenye ukubwa wa mita za mraba 4600 kwa muda mfupi tofauti na hapo awali.

 

"Nilianza kufuatilia hati yangu tangu mwaka 1999 na nimefurahishwa kupata hati ndani ya muda mfupi na sasa natafuta wawekezaji kwenye kiwanja changu nitakaoingia nao ubia ili waweke wananchoweza kuweka ili nipate  kipato cha kunisaidia katika Maisha yangu ya  kila siku". amesema Kabati.