Habari
KILIMANJARO WAANZA KUTUMIA MFUMO WA e-ARDHI
- 21 Sep, 2026
Mkoa wa Kilimanjaro umeanza rasmi utekelezaji wa mfumo mpya wa e-Ardhi baada ya watumishi wa halmashauri saba kupata mafunzo ya siku nane, ikiwa ni miongoni mwa mikoa 11 iliyopewa kipaumbele katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Akizungumzia hatua hiyo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Rehema Mdee, ameeleza kuwa mfumo huo unaondoa urasimu huku ukipunguza gharama za usafiri kwa wanaohitaji huduma za ardhi jambo alilolieleza kuwa, linatimiza maono ya Rais wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Sukuhu Hassan kuwaletea wananchi furaha na tabasamu.
Akigeukia manufaa kwa walio mbali na ofisi za ardhi, Afisa Ardhi Msaidizi kutoka Ofisi ya Msajili Msaidizi wa Hati Mkoa wa Kilimanjaro Bi.Evelina Benedicto Kiyogoma na Afisa Ardhi, Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Luiza Petro Mgungu wameeleza kuwa, mfumo wa e-Ardhi utawasaidia wamiliki wa ardhi wanaoishi nje ya Kilimanjaro kupata huduma bila kufika ofisi za ardhi.
Kwa mujibu wa Mgungu, mwananchi aliye mkoa mwingine wowote anaweza kutuma maombi na kufuatilia kila kitu akiwa huko alipo, jambo alilolieleza kuwa litakamilisha mchakato wa mmiliki wa ardhi kupata hati yake mara baada ya kuwasilisha taarifa sahihi kwenye mfumo.
Kwa upande wa utatuzi wa migogoro ya ardhi Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Bw. Joseph Dickson Mwakasata ameeleza kuwa, wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao 'online' kwa kuweka nyaraka zao.
Mwakasata ameongeza kuwa, mfumo wa e-Ardhi utaongeza uwajibikaji kutokana na viongozi kuweza kufuatilia miamala na kuwachukulia hatua watumishi wanaochelewesha huduma.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Bi.Mdee amehitimisha kwa kueleza kuwa, mfumo huo utapunguza mzigo wa makaratasi ofisini huku watumishi wote wa mkoa huo wake wakithibitisha utayari wao wa kuanza kutoa huduma kikamilifu.