Habari

KIKAO CHA MARIDHIANO CHAFANYIKA MISENYI KUTAFUTA SULUHU YA MGOGORO WA ARDHI

  • 18 Sep, 2026
KIKAO CHA MARIDHIANO CHAFANYIKA MISENYI KUTAFUTA SULUHU YA MGOGORO WA ARDHI

Kikao cha maridhiano cha kujadili na kutafuta suluhu ya changamoto ya ardhi inayowahusisha wananchi, wafugaji na Jeshi kimefanyika leo Sept 17, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Mhe. Kanali Mstaafu Hamis Maiga.

 

Kikao hicho kimejikita katika changamoto inayohusu eneo lililopo Kijiji cha Nkerenge, Kata ya Mtukula, takribani kilomita 30 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Misenyi.

 

Kwa mujibu wa malalamiko yaliyowasilishwa katika kikao hicho, baadhi ya wananchi kutoka Kijiji cha Nkerenge wanadaiwa kuingia katika eneo la Jeshi na kulitumia kwa ajili ya makazi na shughuli za ufugaji.

 

Kutokana na hali hiyo, kikao kimewakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili suala hilo, kupata uelewa wa pamoja kuhusu hali halisi ya eneo hilo na kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za usimamizi wa ardhi.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Mhe. Kanali Mstaafu Hamis Maiga amewataka wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kulifuatilia suala hilo kwa kina na kufanya tathmini ya kitaalamu ili kubaini chanzo na ukubwa wa changamoto hiyo.

 

"Niziombe mamlaka za juu za Wizara ya Ardhi kuingilia kati suala hili ili kusaidia kufanikisha upatikanaji wa suluhu ya kudumu kwa pande zote zinazohusika". amesema

 

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Misenyi, Diwani wa Kata ya Mtukula, wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, mwakilishi wa Jeshi pamoja na wawakilishi wa wananchi wanaohusika na makazi na ufugaji.