Habari

KAZI KUBWA IMEFANYWA NA SERIKALI KATIKA VYUO VYA ARITA NA ARIMO; MZAVA

  • 18 Aug, 2026
KAZI KUBWA IMEFANYWA NA SERIKALI KATIKA VYUO VYA ARITA NA ARIMO; MZAVA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imepokea na kujadili taarifa ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) na Chuo cha Ardhi Mororgoro (ARIMO) ambavyo vipo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na utendaji wa vyuo hivyo.

 

Kikao cha Kamati hiyo kimefanyika Agosti 14, 2026 Bungeni jijini Dodoma kulingana na ratiba iliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Timotheo Mzava.

 

Pamoja na michango ya wajumbe wa Kamati, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe Mzava amesema kazi kubwa imefanywa na Serikali katika kuviboresha vyuo hivyo na kusisitiza, jitihada zaidi kuendelea kuchukuliwa ili kutatua changamoto zinazojitokeza ikiwemo uboreshaji miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kwa lengo la kuandaa wataalamu wa sekta ya ardhi watakaoweza kujiajiri.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa maelekezo yao aliyoyaeleza kuwa, yanalenga kuboresha vyuo hivyo hatua inayosaidia kuongeza udahili wa wanachuo na kuandaa wataalamu wengi zaidi wa sekta ya ardhi nchini.

 

Aidha, kikao hicho cha kamati, kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga, wajumbe wa Menejimenti ya Wizara pamoja na wawakuu wa vyuo hivyo.