Habari

KATIBU MKUU WIZARA YA ARDHI AZINDUA SAMIA ARDHI KLINIKI DODOMA

  • 02 Mar, 2026
KATIBU MKUU WIZARA YA ARDHI AZINDUA SAMIA ARDHI KLINIKI DODOMA

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mha. Anthony Sanga, amezindua rasmi Samia Ardhi Kliniki mkoa wa Dodoma, ikiwa ni mpango maalumu unaolenga kuongeza asilimia ya umiliki wa ardhi kwa wanawake, ambapo kwa sasa takribani asilimia 28 pekee ya wanawake ndio wanamiliki ardhi.

Hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha huduma za ardhi zinatolewa kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa.

Mha. Sanga aliyasema hayo tarehe 02 Machi, 2026 katika Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Kliniki hiyo maalumu mkoani humo itakayofanyika kwa siku sita kuanzia tarehe 02 hadi 07 Machi, 2026.

Alieleza kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ilitambua haki sawa katika umiliki wa ardhi, hata hivyo iliacha nafasi ya kuzingatia mila na tamaduni katika taratibu za kumiliki ardhi hususan kupitia urithi, jambo ambalo kwa baadhi ya makabila limekuwa kikwazo kwa wanawake kupata haki hiyo.

“Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (toleo la mwaka 2023), iliyozinduliwa rasmi Machi 2025 na Mhe. Rais, imefanyiwa maboresho ikiwemo kuondoa vikwazo vya mila na tamaduni vinavyoathiri upatikanaji sawa wa haki ya kumiliki ardhi, hususan kwa wanawake,” alisema Mha. Sanga.

Aidha, alisisitiza kuwa kupitia Samia Ardhi Kliniki, wanawake wanapatiwa huduma mbalimbali ikiwemo elimu na ushauri kuhusu masuala ya ardhi, utoaji wa hati miliki papo kwa hapo, makadirio ya kodi ya pango la ardhi pamoja na huduma nyingine muhimu.

Aliongeza kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta ya ardhi zinatatuliwa kwa wakati na kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mthamini Mkuu wa Serikali wa Wizara hiyo, Bi. Evelyne Baruti Mugasha, alisema hadi majira ya mchana wanawake zaidi ya 160 walikuwa tayari wamejitokeza kupata huduma.

Bi. Mugasha aliwahimiza wanawake wa Mkoa wa Dodoma kutumia fursa ya Kliniki hiyo kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali za ardhi, huku akitoa wito kwa wanaume kutoa ushirikiano ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu.

Wanawake waliopata huduma katika Kliniki hiyo wamepongeza jitihada za Rais Samia kwa kuwapa kipaumbele wanawake katika upatikanaji wa hati miliki ili kuhakikisha hawabaki nyuma kimaendeleo.

Mkazi wa Ilazo, Zena Hamis, alimshukuru Rais Samia kwa kuwapa wanawake kipaumbele na kuwasihi wanawake wote wenye uhitaji wa huduma za ardhi kujitokeza kwa wingi kabla ya Kliniki hiyo kufikia tamati.

Samia Ardhi Kliniki inafanyika katika mikoa yote nchini kuanzia tarehe 02 hadi 07 Machi, 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yatakayofanyika tarehe 08 Machi, 2026, chini ya kauli mbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.”