Habari

KATIBU MKUU ARDHI AIPONGEZA BODI YA CHUO CHA ARDHI TABORA

  • 10 Oct, 2025
KATIBU MKUU ARDHI AIPONGEZA BODI YA CHUO CHA ARDHI TABORA

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameipongeza Bodi ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kufuatia mafanikio na mabadiliko chanya yaliyoonekana chini ya uongozi wa bodi hiyo.

 

Akizungumza na wajumbe wa bodi hiyo aliokutana nao tarehe 9 Oktoba 2025 katika ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma, mhandisi Sanga amesema, ameona mabadiliko makubwa katika utendaji wa bodi ya ARITA jambo alilolieleza limeleta tija na maendeleo ndani ya chuo.

 

"Tumeona mabadiliko makubwa kwenye utendaji na uongozi wa taasisi yenu ndani ya miaka mitatu iliyopita.Mchango wenu umeleta tija na maendeleo, hivyo Wizara imeona ni busara kutoa muda wa nyongeza kwa bodi hii ili muendelee na majukumu yenu muhimu,” alisema Mhandisi Sanga.  

 

Aidha, Mhandisi Sanga amesisitiza umuhimu wa bodi kuendeleza uwajibikaji, weledi, na kuimarisha ushirikiano na Wizara ili kuhakikisha ARITA inazidi kutoa elimu bora ya ardhi kwa manufaa ya taifa.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Lucy Shule, ametoa shukrani kwa Katibu Mkuu huyo kwa kutambua na kuthamini mchango wa wajumbe wa bodi hiyo, na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, bidii na uadilifu mkubwa.