Habari

KATIBU MKUU ARDHI AAGIZA VIKAO VYA MUDA MFUPI OFISI ZA ARDHI KABLA YA KUANZA KAZI

  • 04 Dec, 2024
KATIBU MKUU ARDHI AAGIZA VIKAO VYA MUDA MFUPI OFISI ZA ARDHI KABLA YA KUANZA KAZI

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameziagiza ofisi zote za Ardhi nchini kuanzia mkoa hadi halmashauri kuhakikisha zinakaa vikao vya muda mfupi kila asubuhi  kabla ya kuanza kazi ili kuwa na njia bora ya kutatua changamoto za sekta hiyo.

 

Amesema, utaratibu wa kuwa na vikao vya muda mfupi kila siku  asubuhi kutawawezesha watendaji hao wa sekta ya ardhi nchini kujua namna ya kushughulika na changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika maeneo yao ya kazi.

 

"Mnapokutana mnakaa kwanza vikao vifupi kila subuhi kabla ya kuanza kazi na  kupanga mipango, hata kama kikao cha cha dakika tano ili kuona jana mlifanya kazi vipi na kuna changamoto gani ili mzishughulikie" amesema Mhandisi Sanga.

 

Katibu Mkuu Mhandisi Sanga ametoa maagizo hayo tarehe 2 Desemba 2024 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi ambayo uzinduzi wake utafanyika rasmi

kesho  jumanne tarehe 3 Desemba 2024.

 

Aidha, amewataka watendaji wa sekta ya Ardhi nchini kujitambua na kuelewa kuwa, watumishi wote wa sekta hiyo  ni  wamoja na wananchi wanaelewa kuwa wote ni watumishi wa Ardhi bila kuchanganua taaluma zao.

 

"Unapomuambia mwananchi ramani haijapanda yeye haelewi , usimtume mwananchi bali wewe msaidie, masuala ya ramani ni masuala yenu ya kitaaluma na tutoke katika tabia hiyo na kwenda kusaidia wananchi" amesema Mhandisi Sanga.

 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara hiyo  hatua kali zitachukuliwa kwa watumishi wa sekta ya ardhi watakaochelewesha huduma kwa makusudi.

 

"Hili ni jambo tunalolipiga vita sana, ni wasihi wakuu wa Idara kukagua kazi za wasaidizi wao kama ni kazi ikipokelewa itolewe".

 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi SMZ  Bi Mhaza Gharib Juma amesema, Wiki ya Ardhi inayoadhimishwa  itaimarisha mashirikiano baina ya Zanzibar na Tanzania Bara katika masuala ya sekta ya ardhi hasa ikizingaitiwa lengo kuu la serikali zote mbili ni kuisaidia jamiii.

 

Aidha, ametaka kuangalia namna sekta ya ardhi itakavyoweza kuimarisha masuala ya uwekezaji nchini kwa kuwa ardhi ni kila kitu  na kusisitiza kuwekwa mikakati imara itakayoweza kutumia ardhi kwa uadilifu na haki ili kuimarisha uwekezaji na kupata fedha zitakazoongeza huduma mbalimbali kwa jamii.

 

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaadhimisha Wiki ya Ardhi  kuanzia tarehe 2 hadi 5 Desemba 2024 ambapo mbali mambo mengine wiki hiyo inatumika kujadili utoaji huduma za kisekta pamoja na uwepo mawasilisho mbalimbali  kwa lengo la kufanya maboresho ya maeneo yenye changamoto.