Habari

KAMATI YA BUNGE YASISITIZA WANANCHI KUELIMISHWA UMUHIMU WA HATIMILIKI ZA ARDHI

  • 26 Oct, 2026
KAMATI YA BUNGE YASISITIZA WANANCHI KUELIMISHWA UMUHIMU WA HATIMILIKI ZA ARDHI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imesisitiza umuhimu wa wananchi kujengewa uelewa wa umuhimu wa kuwa na Hatimiliki za Ardhi katika maisha yao.

 

Wito huo umetolewa Oktoba 21, 2026, jijini Dodoma, wakati Kamati hiyo ilipopokea na kujadili Taarifa ya Hali ya Upimaji na Umilikishaji wa Ardhi nchini iliyowasilishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 

Taarifa hiyo imewasilishwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana, Dkt. Leonard Akwilapo.

 

Katika majadiliano hayo, wajumbe wa Kamati wameitaka Wizara kuendelea na juhudi za kusambaza Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Ardhi (e-Ardhi) katika mikoa yote nchini ili kurahisisha utoaji huduma za ardhi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hizo.

 

Akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo, Naibu Waziri Mhe. Mmuya amesema Mfumo wa e-Ardhi umeanza kutumika katika mikoa 17 nchini.

 

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Dodoma, Tanga, Mwanza, Mbeya, Singida, Kilimanjaro, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Kagera pamoja na mkoa wa Njombe.

 

Naibu Waziri Mmuya aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, Kamishna wa Ardhi, Bw. Mathew Nhonge; wajumbe wa Menejimenti ya Wizara pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.