Habari

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TUME YA MATUMIZI YA ARDHI

  • 26 Oct, 2026
KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TUME YA MATUMIZI YA ARDHI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeonesha kuridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, huku ikisisitiza umuhimu wa kukamilisha hatua zote za upangaji wa matumizi ya ardhi.

 

Kauli hiyo imetolewa leo, Oktoba 22, 2026, jijini Dodoma, wakati Kamati hiyo ilipopokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi.

 

Akizungumza baada ya kupokea na kujadili taarifa hiyo pamoja na majibu ya hoja mbalimbali zilizotolewa na wajumbe wa Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga, Mhe. Timetheo Mzava, amesema Kamati imeridhishwa na namna Tume inavyotekeleza majukumu yake licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

 

“Pamoja na changamoto kama vile fedha na vitendea kazi, Tume imefanya kazi zake vizuri. Kikubwa ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu yake unakamilika hadi hatua ya mwisho, ikiwemo utekelezaji wa hatua zote sita za upangaji wa matumizi ya ardhi,” amesema Mzava.

 

Aidha, Mzava amesema licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kushughulikia changamoto za ardhi nchini, migogoro ya ardhi bado ni mingi inayohitaji mikakati madhubuti ya kuitatua.

 

Amesema, Kamati yake ya Kudumu ya Bunge inaendelea kutafakari namna bora ya kukabiliana na migogoro hiyo ili kusaidia kuboresha usimamizi wa ardhi na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.

 

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo aliyeambatana na Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga pamoja na Menejiment ya Wizara aliahidi kuzinyia kazi hoja zote zilizowasilishwa kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi.