Habari

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ARDHI VIJIJINI

  • 13 Nov, 2023
KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ARDHI VIJIJINI

Na Hassan Mabuye, Simiyu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika vijiji vya Mwadila, Zabazaba na Igongwa katika halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.

Akieleza mbele ya wakazi wa vijiji hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mzava wakati wa Ziara ya kamati hiyo wilayani humo amesema ni jambo la kuipongeza Wizara ya Ardhi katika kuwezesha mradi huo kuweka mazigira mazuri ya matumizi bora ya ardhi.

Amesema kuwa kazi ya kamati hiyo ambayo wamekuja kuifanya ni kufuatilia na kujiridhisha fedha zilizotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu baada ya kupitishwa na bunge ili kutekeleza mradi huo zilizotengwa kwa wilaya ya Maswa zimefika na zimefanya kazi iliyokusudiwa.

Amesema kuwa kulingana na maelezo waliyoyapata kutoka kwa watekelezaji wa mradi huo pamoja na wananchi wa vijiji hivyo sambamba na kuonyesha ramani zilizotengwa kwa ajili ya kuonyesha matumizi bora ya ardhi kwa pamoja wamejiridhisha kuwa kazi imefanyika vizuri.

 "Kazi yetu sisi kamati hii ya bunge ambayo imetufikisha wilayani Maswa ni kufuatilia na kujiridhisha fedha zilizotolewa na bunge zaidi ya Tsh.  Bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu katika wilaya hii zimefika na kufanya kazi iliyokusudiwa kwa ufanisi.

"Maelezo tuliyopewa na watendaji wa serikali wanaotekeleza mradi huu na yale mliyoyatoa ninyi wananchi na mawasilisho kwetu kupitia ramani tumejirisha  sisi kama kamati kuwa kazi imefanyika vizuri."amesema.

Amesema kwa kuwa mradi huo  unatekelezwa na serikali kwa kupitia wizara ya ardhi na wananchi wameshirikishwa ni mradi mzuri ambao unafaida nyingi zikiwemo kuondoa tatizo la migogoro ya mipaka katika ya Kijiji na Kijiji, mipaka ya mashamba sambamba na kuongeza thamani ya Ardhi.

Ameendelea kueleza kuwa mipango ya ardhi  iliyowekwa katika maeneo ya vijiji ni vizuri yakatumika kama walivyoonyesha kwenye ramani ya kila kijiji kulingana na makubaliano yenu na siyo kubadilisha matumizi.

'Katika mipango yenu mliyoweka kama kijiji mkakubaliana kutenga maeneo mathalani eneo litumike kama eneo la akiba, eneo la kilimo, eneo la kuchungia ni vizuri likatumika kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Geophrey Pinda amesema  kuwa wilaya hiyo inakwenda kupima vijiji vyote 120 kwa mchanganuo kuwa vijiji 106 vitapimwa, Vijiji 5 vitaingizwa katika mji wa Maswa na vijiji 9 vitapewa hadhi ya kuwa miji midogo na wananchi watapatiwa Hati Milki za Ardhi.

Amesema kuwa mradi huo utakuwa endelevu na moja ya  umuhimu wa kupima miji ni kuweka matumizi bora ya ardhi na kuondoa changamoto zilizokuwa zinajitokeza za migogoro ya ardhi ya mara kwa mara.

"Tunapopima ardhi hivi tunaondoa migogoro  ya ardhi ambayo imekuwa mingi katika jamii na hii ndiyo dawa yake na hapa Maswa tumeweza kutenga Hekta 77,000 kwa ajili ya kilimo cha Umwagiliaji, Hekta 481 kwa ajili ya taasisi za serikali na Hekta 713 kwa ajili ya kuweka Viwanda na Uwekezaji,"amesema.

Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais  Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuona ipo sababu ya kuleta mradi huu katika Wilaya hiyo kwani ni mradi wenye tija kwa wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Afisa Ardhi wilaya ya Maswa,Vivian Christian amesema kuwa muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miaka mitano kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka 2027, kwa halmashauri hiyo ulianza mwezi Februari mwaka  huu na utatumia zaidi ya Tsh.Bilioni tatu.

Amesema kuwa mradi huo tangu uanze kutekelezwa na kukamilika kwa baadhi ya vijiji umekuwa suluhisho la kuongeza usalama wa haki za ardhi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ardhi na utatuzi wa migogogo.

"Mradi huu utakuza uwekezaji katika sekta ya ardhi hapa wilayani Maswa na kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi katika usimamizi wa ardhi yao kwa maendeleo endelevu,"amesema.