Habari
KAMATI YA BUNGE YAKAGUA MRADI WA NHC WA BILIONI 8.6 MKWAKWANI TANGA
- 18 Mar, 2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa saba la makazi na biashara unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Mkwakwani, Jijini Tanga.
Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 17 Machi 2026 na kuongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mzava (Mb.), ikiwa ni sehemu ya majukumu ya kamati ya kusimamia na kukagua utekelezaji wa miradi pamoja na matumizi ya fedha za Serikali.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi. Dkt. Batilda Burian na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng. Anthony Sanga, Kamishna wa Ardhi Nathaniel Mathew pamoja na wataalamu mbalimbali wa sekta ya ardhi walishiriki katika ukaguzi huo.
Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 8.6 ambapo unatarajiwa kukamilika mwaka 2027, ikielezwa kuwa kukamilika kwa Ujenzi huo kutachangia kuongeza upatikanaji wa makazi bora pamoja na maeneo ya biashara sambamba na kuendeleza ukuaji wa uchumi wa Jiji la Tanga.